Amira afunguka alivyopoteza mimba baada ya kupigwa na aliyekuwa mume wake, Jimal Rohosafi

Amira amemshutumu aliyekuwa Jimal kwa kuwa mtu mkatili

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili alidai kwamba Jimal alimshambulia na kumpiga mara kadhaa wakati wa ndoa yao.

•Amira alisema kwamba kabla ya kuamua kutoroka ndoa yake na Jimal, aliteseka kihisia, kimwili na hata kisaikolojia.

Amira, Jimal Rohosafi
Image: INSTAGRAM//

Mfanyibiashara mashuhuri, Amira, amemshutumu aliyekuwa mume wake, Jimal Marlow Rohosafi, kwa kuwa mtu mkatili.

Huku akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, mama huyo wa watoto wawili alidai kwamba Jimal alimshambulia na kumpiga mara kadhaa wakati wa ndoa yao.

Amira alifichua kwamba kisa cha mwisho kilitokea katika nyumba yao mwaka wa 2021 na hata kumfanya apoteze ujauzito.

"Hilo lilikuwa tukio la hivi punde, acha nisiongee jinsi alivyokuwa akinipiga nikiwa na ujauzito wa mtoto wangu Amir wa miezi tisa... Safari hii alinipiga mbele ya watoto wangu, wazazi wake na familia yake na wakasimama pale kwa kweli wakimchochea ili anipige na hapo ndipo nilipomaliza (Mimba iliharibika)," alisema.

Mfanyibiashara huyo alisema kisa hicho kilitokea wakati wa sherehe ya harusi ya dadake Jimal iliyokuwa ikifanyika nyumbani kwao.

Amira alisema kwamba kabla ya kuamua kutoroka ndoa yake na Jimal, aliteseka kihisia, kimwili na hata kisaikolojia.

"Najua baadhi yenu mlikuwepo siku hiyo. Mnaweza kuja na kuthibitisha kama hii ni kweli. Laiti ningeweza kuandika kila kitu nilichopitia na mwanamume huyu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ilikuwa ni unyanyasaji wa kiakili, kimwili na kihisia," alisema.

Mama huyo wa wavulana wawili alisema kuwa Jimal ndiye mwanaume mbaya zaidi amewahi kukutana naye maishani. Alikiri chuki yake kubwa kwa mzazi huyo mwenzake na kubainisha kuwa daima hatawahi kumsamehe.

Amira alibainisha kuwa alivumilia ndoa sumu na Jimal Rohosafi kwa miaka mingi kwa ajili tu ya ustawi wa watoto wao.

"Nilikaa kwenye ndoa yenye sumu kwa sababu yao, nilishikilia ndoa ambayo tayari ilikuwa imevunjika. Alikuwa mtu mbaya zaidi ambaye nimewahi kukutana naye na ninamchukia sana, sitamsamehe kamwe, na hata kama nitakufa leo (Mungu tu anajua ni lini) nisingependa anizike au hata kuniomboleza,” alisema.

Alibainisha kuwa hajutii kamwe kugura ndoa hiyo na hata akasema kwamba anatamani angeondoka mapema.

"Nipo na raha mahali nilipo sasa," alisema.

Ndoa ya Jimal na Amira ya muda mrefu ilisambaratika mwishoni mwa mwaka 2021 baada ya Jimal kuonekana kumchagua aliyekuwa mkewe wa pili, mwanasoshalaiti Amber Ray, badala ya mkewe wa kwanza.