Bungoma: Mwanamume amaliza ugali kilo 2 kwa dakika 35

Washiriki katika mchezo huo wa kujifurahisha walisema kuwa waliamua tu kushindana na kabla ya kushirika huwa wanashinda njaa.

Muhtasari

• “Tulisema wacha tulete tu mahindi tupike ugali tushindane tuona nani ataibuka mshindi" - Alisema.

Mwanamume mmoja katika kaunti ya Bungoma amegonga vichwa vya habari baada ya kuibuka mshindi katika shindano la kula ugali.

Inaarifiwa kwamba mwanamume huyo aliibuka mshindi baada ya kumaliza kula ugali kilo mbili ndani ya dakika 35 tu.

Katika video ambayo ilipakiwa na runinga ya K24, mwanamume huyo ambaye hakutambuliwa kwa jina anaonekana akiwa miongoni mwa wanaume wengine wakimenyana katika ufundi wa mdomoni.

“Tulisema wacha tulete tu mahindi tupike ugali tushindane tuona nani ataibuka mshindi. Huu mchezo umeanza kitambo tu haujaanza leo, huwa hatuli nyumbani, tunakuja hapa tunashinda njaa kabla ya mashindano,” wakaazi wa eneo hilo walisema.

Mashindano ya ulaji si mageni katika jamii nyingi Afrika kwani wiki jana, tuliripoti kuhusu shindano la Tonge Nyama ambalo lilifanyika nchini Tanzania, Morogoro.

Katika shindano hilo ambalo lilikuwa la pesa, mkaazi mmoja aliibuka mshindi baada ya kumaliza wali kilo 2 na maji lita moja ndani ya dakika 8 tu.

Mkaazi huyo aliyetambuliwa kwa jina David, alitunukiwa shilingi laki moja pesa taslimu za Tanzania baada ya kuwabwaga wenzake, n ahata kuonekana akijaribu kutoa msaada kwa wenzake ambao walionekana kulelewa na wali huo.

Wakaazi walisema kwamba mchezo huo wa kula hufanyika mara kwa mara na dhima yake ni kurai wananchi kudumisha Amani na usalama, na pia kutambua utamaduni wao.