Daddy Owen afunguka kwa nini hajapata mapenzi tena baada ya ndoa yake kuvunjika

Mwimbaji huyo alifichua kwamba wanawake wengi humtumia jumbe za mapenzi na picha za uchi.

Muhtasari

•Owen alisema aliamua kujiangazia mwenyewe baada ya kuenda njia tofauti na aliyekuwa mkewe, Farida Wambui.

•Mwimbaji huyo alibainisha kuwa yeye ni mtu mashuhuir na mara nyingi huwa anatongozwa na wanawake.

Image: INSTAGRAM// DADDY OWEN

Mwimbaji mkongwe wa nyimbo za injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen amefichua kwa nini bado hajajitosa kwenye ndoa nyingine, takriban miaka mitatu baada ya ndoa yake ya kwanza kuvunjika.

Akizungumza kwenye mahojiano na Shaffie Weru, mwanamuziki huyo alibainisha kuwa kupata mapenzi sio tatizo kwake

Owen aliweka wazi kwamba aliamua kujiangazia mwenyewe baada ya kuenda njia tofauti na aliyekuwa mkewe, Farida Wambui.

"Nilisema niende, nijifanyie kazi, nibadilishe mambo kadhaa alafu baada ya hapo mambo mengine yatafuata," alisema.

Kaka huyo wa mwimbaji Rufftone alibainisha kuwa yeye ni mtu mashuhuir na mara nyingi huwa anatongozwa na wanawake.

Owen alifichua kwamba kuna wanawake wengi ambao humtumia jumbe tamu za mapenzi wakilenga kuchumbiana naye huku wengine wakitumtumia picha za uchi wao wakikusudia kumtongoza.

"Tushazoea, ziko nyingi. Kwanza huwa nawablock mara moja," alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 41 alifichua kuwa wanawake walijaribu kumtongoza baada ya ndoa yake kuvunjika mwaka wa 2020. Alisema alipokea jumbe nyingi haswa kwenye mtandao wa Instagram.

Kwenye mahojiano na Plug TV mwaka jana, mwanamuziki huyo mahiri alidokeza kuwa tayari amemsamehe aliyekuwa mke wake, Farida Wambui kufuatia kutengana kwao takriban miaka mitatu iliyopita.

Owen hata hivyo aliweka wazi kuwa tangu wakati huo amesonga mbele na maisha yake na kudokeza kuwa si rahisi kwa wao kurudiana.

"Mimi ni mtu ambaye kitu ikifanyika nakusamehe lakini nasonga mbele. Kusonga nitasonga, lakini kusamehe nitasamehe," alisema.

Owen na mkewe wa kwanza Farida Wambui walitengana mwishoni mwa mwaka wa 2020 baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na masuala ya kutokuwepo kwa uaminifu katika ndoa.

Kwenye mahojiano hayo, msanii huyo wa injili aliweka wazi kwamba yuko bize na mambo tofauti na hivyo hajapata muda wa kujikita katika kutafuta suluhu ya mzozo wake na mke wake wa zamani, Bi Wambui.

Pia alikana madai kuwa yuko chini ya shinikizo la kutafuta mke na kuweka wazi kuwa kwa sasa hata hatafuti mchumba.

"Mimi ni mwanaume, siwezi kutangaza eti natafuta mwanamke. Nikitaka mwanamke nitampata. Mimi ni simba, nitaenda niwinde na nimpate nimtakaye," alisema.

Owen alisisitiza kwamba jambo kuu ambalo atakuwa akilizingatia kwa mwanamke atakapokuwa katika pilkapilka za utafutaji ni sifa ya kumcha Mungu.

Pia alibainisha ni sharti atakayekuwa mkewe awe amelelewa kijijini.