Jinsi Guardian Angel alivyosherehekea mwanawe wa kambo, Glenn Naibei akitimiza miaka 25

Katika jibu lake, Glenn alisema, "Asante G wangu."

Muhtasari

•Guardian Angel ni miongoni mwa waliomsherehekea Glenn Naibei  kwa kumtakia heri katika siku yake ya kuzaliwa.

•Esther Musila alimtakia baraka nyingi mwanawe na kumtia moyo kuendelea kupambana maishani kwa ujasiri.

Guardian Angel, mkewe Esther Musila na Glenn Naibei
Image: INSTAGRAM

Mnamo Ijumaa, Juni 2, mmoja wa watoto watatu wa Esther Musila, Glenn Naibei aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Wanafamilia, marafiki na wanamitandao wengine walimsherehekea Glenn kwa jumbe nzuri huku akitimiza umri wa miaka 25. Mume wa mamake, mwanamuziki Guardian Angel ni miongoni mwa waliomsherehekea kwenye mitandao ya kijamii kwa kumtakia heri katika siku yake ya kuzaliwa.

“Baraka za siku ya kuzaliwa my G @__jama1,” Guardian Angel aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuambatanisha na picha ya mkewe na Glenn.

Katika jibu lake, Glenn alisema, "Asante G wangu."

Huku akimsherehekea mwanawe, Esther Musila alimtaja kama mtu wa kupendeza, mwenye moyo mkunjufu, mwenye mawazo makubwa, anayeaminika na aliyejawa na upendo.

Musila alimtakia baraka nyingi mwanawe na kumtia moyo kuendelea kupambana maishani kwa ujasiri.

"Glenn, ni siku yako maalum na ninakutakia kipande kikubwa zaidi cha furaha leo. Siku hii ya kuzaliwa na iwe ukumbusho wa kila wakati kujitahidi kupanda mlima wowote unaosimama kwenye njia yako na Mungu Mwenyezi aongoze hatua zako,” Musila alimwandikia Glenn kwenye ukurasa wake.

“Ubaki na nia. Tunakutakia ujasiri na dhamira na uwe na mwaka mzuri na maisha matukufu mbeleni. Daima tuko pamoja nawe. Heri ya kuzaliwa. Tunakupenda na wewe ni maalum kwetu. Furahia siku yako G.

Glenn alijibu kwa kumshukuru mama yake na kuonyesha upendo wake mwingi kwake.

Kijana huyo ni mmoja wa watoto wa Bi Esther Musila kutoka kwa ndoa yake ya awali. Ana mtoto mwingine wa kiume na wa kike kwa jina Kim na Gilda Naibei.

Esther Musila ,53, alijitosa kwenye ndoa yake mpya na Guardian Angel ,35, mwezi Januari mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa takriban miaka miwili. Wawili hao hata hivyo hawana mtoto pamoja.

Mwaka jana, mwanamuziki Guardian Angel aliweka wazi kuwa kupata watoto sio kipaumbele katika ndoa yake na Esther Musila.

Katika mahojiano ya Juni, mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili alisema nguzo kuu uhusiano wao ni mapenzi na si watoto.

Guardian Angel alisema kwamba kupata mtoto na Bi Musila ni la ziada kutoka kwa Mungu  ambayo kwake si lazima wapate.

 "Nilipoingia kwenye ndoa yetu, mtoto ni nambari mbili. Akija ama akose ni sawa. Nambari moja ni upendo wetu. Mungu akitaka kutupatia bonasi ya baraka ya mtoto ni sawa. Lakini kama haipo, hiyo ni bonasi, tunafurahia na tulicho nacho. Upendo wetu ndio ninaojali," Guardian alisema katika mahojiano na Plug TV.

Mwanamuziki huyo alisema upendo wao pekee umetosha na kueleza kuwa umemletea amani kubwa moyoni.

"Tukipata mtoto ni sawa, tukikosa pia haipunguzi chochote kwa upendo wangu kwa mke wangu," Alisema.