Muziki wa Genge kujumuishwa kwenye tuzo za Grammy

Kitengo hiki kipya kinajumuisha aina mbalimbali za muziki, zikiwemo Genge,Afrobeat, Afro-fusion, Amapiano, Bongo Flava.

Muhtasari

• Kitengo hiki kitasherehekea muziki kuonyesha utamaduni na maisha ya Afrika.

• Hakuna msanii wa Kenya ambaye amewahi kuzishinda tuzo za Grammy tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo.

Tuzo za Grammy zimejuimuisha muziki wa Genge kama kitengo kipya cha muziki wa Afrika .

Chuo cha Kurekodi cha Tuzo za Grammy kimetoa tangazo muhimu ambalo limeleta msisimko katika sekta ya muziki kote Afrika.

Tuzo za Grammy za 2024 zitakuwa na vipengele vitatu vipya, huku kinachotarajiwa zaidi kikiwa "Best African Music Performance." Kitengo hiki kitasherehekea miziki zitakazoonyesha utamaduni na maisha ya Afrika.

Kitengo kipya kilichoanzishwa kinalenga kutuza sauti na midundo ambapyo hutofautiana katika bara zima.

Kitengo hiki kipya kinajumuisha aina mbalimbali za muziki, zikiwemo Genge, Afrobeat, Afro-fusion, Afro-Pop, Alte, Amapiano, Bongo Flava, Kizomba, Chimurenga, High Life, Fuji, Kwassa, Ndombolo, Mapouka, Ghanaian Drill, Afro- House, Hip-Hop ya Afrika Kusini, na Ethiopia Jazz.

Mbali na kitengo bora cha muziki bora wa Kiafrika, taasisi hiyo ya Grammy pia kimetambulisha kitengo cha "Best Alternative Jazz Album" na "Best Pop Dance Recording". Upanuzi huu unaonyesha kujitolea kwa Grammy kutambua aina mbalimbali za muziki.

Hatua hii ya tuzo za Grammy ni ushindi mkubwa katika kuendeleza muziki wa bara la Afrika kwa jumla na hasaa kwa wasanii wa Kenya amabao wanafahamika kwa muziki wa Genge.

Kumekuwa na gumzo na mjadala mitandaoni kuhusiana na wasanii na miziki ya Kenya kukosa kutambuliwa nje ya mipaka ya Kenya.

Baadhi ya wasanii wa Kenya wamesherehekea hatua hii wakiwemo Mandy, Mejja,Dj Joe Mfalme, Victoria Kimani na wengine wengi.

Ujumbe wa Mejja ulisoma, “ Respect to my Godfathers Jua Cali na Clemo na mbogi ya Calif mliona vision tukasonga nayo wengi wakatukanwa tukazidi Mungu halali tumekufa nayo na tutazikwa nayo. Genge ni muziki wa umati wagenge tuzidi Jahbless.”

Hakuna msanii wa Kenya ambaye amewahi kuzishinda tuzo za Grammy tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo.