Harmonize amlilia Hamisa Mobetto am'cheat mpenziwe, amruhusu kuwa mpango wake wa kando

Harmonize anamwambia Hamisa kuwa anafahamu ana mpenzi lakini anamsihi asimnyime nafasi moyoni mwake.

Muhtasari

•Harmonize amemsihi mwanamitindo Hamisa Mobetto ampe nafasi moyoni mwake licha ya kuwa tayari yuko kwenye mahusiano mengine.

•"Je, huoni sura yako nzuri kwenye wallpaper yangu? Hiyo ina maana niko tayari kukupa karatasi yangu yote," Harmonize anaimba.

Image: INSTAGRAM

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amemsihi mwanamitindo Hamisa Mobetto ampe nafasi moyoni mwake licha ya kuwa tayari yuko kwenye mahusiano mengine.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide ameachia wimbo mpya ambapo anamwambia mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz kwamba yuko tayari kuwa mpango wake wa kando. Ingawa hataji jina lake waziwazi katika wimbo huo, mtu anaweza kujua wazi kwamba maneno hayo yanaelekezwa kwa mama huyo wa watoto wawili.

Katika wimbo huo, mwimbaji huyo anamwambia Hamisa Mobetto anafahamu fika kwamba ana mpenzi lakini anamsihi kutoruhusu uhusiano wake na Mtogo Kevin Sowax usimnyime nafasi katika maisha yake.

"Sijui kama ni wakati mwafaka wa kusema hivi. Ninachojua ni kwamba sina budi kukuambia hili. Umbo lako la mwili linanifanya nifanye hivi. Je, unaona? Mpenzi natumai unajua hili. Najua una mwanaume. Unaonekana unaenda kuwa mke wa mtu. Naweza kuwa mtu wako bora. Usinipoteze, nifanye tu mpango wako wa kando,” Konde Boy anaimba katika wimbo huo ambao aliachia mwishoni mwa wiki iliyopita.

 Anaendelea, "Je, huoni sura yako nzuri kwenye wallpaper yangu? Hiyo ina maana niko tayari kukupa karatasi yangu yote (Baby karatasi yangu yote). Acha niwe mpango wako wa kando (x5). Nataka kuwa mpango wako wa kando. Mpenzi nifanye kuwa mpango wako wa kando. Naapa nasubiri hadi uwe wangu."

Wimbo huu unakuja siku chache tu baada ya mastaa hao wawili kudokeza kuhusu uhusiano wao kuvurugika.Hii ilionyeshwa na maendeleo ya hivi majuzi ambapo wote waliacha kufuatiliana kwenye mtandao wa Instagram. Walikuwa wakifuatiliana kwa muda mrefu na hata kutajana mara kwa mara kuonyesha urafiki wao.

Hatua hii ilikuja siku chache baada ya mpenzi wa Hamisa Mobetto, Kevin Sowax kuwasili nchini Tanzania kwa mara ya kwanza na kukiri kuwa hata hamfahamu bosi huyo wa Konde Music Worldwide ambaye anadai kuwa rafiki mkubwa wa mpenzi wake.

"Simjui, simjui," Kelvin alisema katika mahojiano wakati alipoulizwa ikiwa anafahamu urafiki wa Harmonize na mpenzi wake.

Ugomvi kati ya Hamisa na Harmonize huenda ulishika moto takriban wiki moja iliyopita baada ya bosi huyo wa Kondegang kuzungumza vibaya kuhusu mpenzi wa Hamisa akijigamba kuwa tajiri kuliko yeye kwa mbali sana.

Wakati akijibu madai ya mtangazaji Juma Lokole kwamba hawezi kushindana na Kevin katika masuala ya fedha, Konde Boy alisema kuwa mifuko yake imesheheni zaidi ya Mtogo huyo.

Bosi huyo wa Konde Music Worldwide alidokeza kuwa njia mojawapo ya kulinganisha utajiri wao ni kuangalia aina ya gari kila mmoja anamiliki.

“Ingawa mimi sio mtu wa kuongelea maisha ya watu nisiowajua lakini niamini niko na hela nyingi kuliko jamaa huyo. Kabla hujamnunulia mwanamke gari inatakiwa tujue unaendesha gari ganii!! Au ndio hayanihusu. Si tushavuka kwenye magari,” Harmonize alisema katika taarifa kwenye Instastori zake.

Ili mfanyibiashara huyo wa Togo kudhihirisha kuwa yeye ni tajiri sana kama inavyodaiwa, Harmonize amemtaka amnunulie Hamisa nyumba.

"Kama hawezi, basi nitamuonyesha jinsi tulivyo serious na marafiki zetu wakubwa, sisi wanaume wa Kitanzania!! Kwenye magari tushavuka,” alisema.