"Unafanya bedroom maandamano!" Kabi Wajesus alalamika kuhusu mkewe kunyamba sana kitandani

Kabi alifichua kuwa mkewe huchafua hali ya hewa sana usiku wakati akiwa amelala.

Muhtasari

•Kabi alitoa ombi kwa Milly kupunguza kufanya kitendo hicho hata kama ni sawa kwa sababu tayari wamezoeana.

•Katika utetezi wake, Milly Wajesus alisema kuwa wataalam wanashauri watu kuharibu hewa takriban mara 18 hadi 22 kwa siku.

Milly na Kabi Wajesus
Image: INSTAGRAM// THE WAJESUS FAMILY

Mwanavlogu maarufu Peter Kabi almaarufu Kabi Wajesus ameibua wasiwasi kuhusu mkewe Milly Wajesus kuchafua hali ya hewa usiku wakiwa wamelala.

Katika mazungumzo yao ambayo walipakia kwenye chaneli yao ya YouTube, Kabi alifichua kuwa mkewe huchafua hali ya hewa sana usiku wakati akiwa amelala.

Kufuatia hilo, mtumbuizaji huyo alitoa ombi kwa mama huyo wa watoto wake wawili kupunguza kufanya kitendo hicho hata kama ni sawa kwa sababu tayari wamezoeana.

“Ni sawa kunyamba mara moja moja, lakini mpenzi tafadhali nakuuliza, unaweza kuacha kuninyambia kwa kitanda? Inaweza kudhibitiwa, mbona mimi huwa sinyambi?” Kabi alilalamika kwenye video ya mazungumzo yao waliyoshiriki Jumanne.

Mwimbaji huyo wa zamani ambaye kwa sasa ni muumini mkubwa alimbainishia Milly kuwa ni sawa na kuharibu hali ya hewa wakati wa mchana kwani kuna uhuru wa nafasi tofauti na wanapokuwa kitandani usiku ambapo mtu hawezi kutoroka harufu mbaya.

“Huo ni unyanyasaji kwa sababu sina pa kwenda. Kusema kweli, kuna baridi sana Kiambu huwa nafunika kichwa changu. Unaniua! Ninaamka kama mabomu ya machozi. Unafanya chumba cha kulala cha maandamano kila wakati,” Kabi alilalamika.

Katika utetezi wake, Milly Wajesus alisema kuwa wataalam wanashauri watu kuharibu hewa takriban mara 18 hadi 22 kwa siku.

Mama huyo wa watoto wawili pia alibainisha kuwa Kabi pia yeye hufanya hivyo sana licha ya kumlalamikia.

"Hilo ni jambo ambalo siwezi kudhibiti. Mimi ni kawaida kulala. Sio kwamba ninaamua tu kuifanya, " alisema.

Wanandoa hao walifichua kuwa katika siku za nyuma walikubali kuacha tabia hiyo wakiwa kitandani baada ya Milly kufanya hivyo kwa usiku mzima.

Kabi alisema mwanzoni alidhani ni sawa na ni jambo la kufurahisha kwa sababu tayari wameshazoea lakini alikuja kuacha, hata hivyo mkewe hakuwahi kubadilika kwa upande wake.

"Siyo haki," Kabi alisema.

Milly alisema kuwa hilo linaweza kuwa tatizo kwenye mfumo wake wa usagaji chakula na kumtaka mumewe kuzoea kwani ni sehemu ya ndoa.