Bahati, Terence Creative watoa kauli baada ya akaunti ya Andrew Kibe ya YouTube kufungwa

Akaunti ya YouTube ya Kibe yenye wafuasi wengi ilifungwa Jumatatu.

Muhtasari

•Bahati na Terence wamekuwa wahasiriwa wakubwa wa kejeli za Kibe huku mara nyingi akiwaita ‘Kabahanye’ na ‘Nganuthia.’ mtawalia.

• Terence alibainisha kuwa chaneli ya Kibe ya YouTube ilikuwa ya manufaa kwake kinyume na walivyofikiri wengi.

Terence Creative, Andrew Kibe, Bahati
Image: HISANI

Wasanii maarufu wa Kenya, Kelvin Bahati na Terence Creative wameshiriki maoni yao baada ya akaunti ya YouTube ya mtumbuizaji Andrew Kibe kufungwa.

Bahati na Terence wote wamekuwa wahasiriwa wakubwa wa kejeli za Kibe huku mburudishaji huyo mara nyingi akiwaita ‘Kabahanye’ na ‘Nganuthia.’ mtawalia.

Mara tu baada ya habari za kufungwa kwa chaneli ya mtangazaji huyo wa zamani siku ya Jumatatu jioni, Terence alielezea kusikitishwa kwake na hatua hiyo.

"Inasikitisha sana, nitakosa viboko vya Nganuthia," Terence alisema.

Siku ya Jumanne, Bahati alishiriki video ya Terence na mke wake Milly Chebby wakibusiana na kudokeza kwamba wapenzi hao sasa wanaweza kufurahia uhusiano wao kwa amani.

Mwanamuziki huyo alidokeza kuwa sio tu Terence na Milly Chebby ambao watafurahia, lakini pia yeye atapata kusherehekea penzi lake na Diana Marua kwa amani.

“Naskia sasa Nganuthia na Kabahanye wanaweza kusherehekea wawapendao kwa amani. Terence Creative na Milly Chebby wamethibitisha #HUYU ni kibao kali,” Bahati aliandika chini ya video aliyochapisha kwenye Instagram.

Huku akijibu maoni kuhusu chapisho la Bahati, Terence alibainisha kuwa chaneli ya Kibe ya YouTube ilikuwa ya manufaa kwake kinyume na walivyofikiri wengi.

"Hapana hatufanyi hivyo(kusherehekea), jukwaa hilo lilikuwa na manufaa zaidi kwangu kuliko wewe," Terence alimjibu mtumizi wa Instagram.

Akaunti ya YouTube ya Kibe yenye wafuasi wengi ilifungwa Jumatatu.

Taarifa ya kuhusu hatua hiyo iliyoonyeshwa kwenye akaunti hiyo ilisoma, "akaunti ya YouTube inayohusishwa na video hii imesimamishwa." .

Siku za hivi majuzi, mtumbuizaji huyo ambaye kwa sasa yuko nchini Marekani amekuwa akiwajulisha mashabiki wake kwamba mara tu atakapomaliza kutumia mtandao wa YouTube, atapakia maudhui yake kwenye jukwaa lingine.

Hivi ndivyo maelezo ya wa Google yanasema kuhusu akaunti ya YouTube kufungwa;

•Iwapo jukwaa lako lilikatishwa kwa sababu ya madai ya ukiukaji wa hakimiliki na unadhani madai hayo si sahihi, unaweza kuwasilisha arifa ya kukanusha. Mchakato huu bado unapatikana kwa watayarishi walio na akaunti zilizofungwa, lakini fomu ya wavuti ya arifa ya kukanusha haitapatikana.

•Je, kufutwa kwa akaunti ya YouTube ni kwa kudumu? YouTube inaweza kusimamisha akaunti, kwa muda au kabisa, kutoka kwa huduma zao za mitandao ya kijamii.

•YouTube inaweza kusimamisha akaunti yoyote wanayochagua kuifunga bila kuhitaji kutoa sababu yoyote.

•Unaweza kukata rufaa kwa kuunda na kuwasilisha rufaa ya video au kwa kuwasiliana na Usaidizi kwa Watayarishi kutoka ndani ya Studio ya YouTube. Baada ya kuwasilisha rufaa yako, timu zetu zitajibu ndani ya siku 14 na kutoa uamuzi.