Mwanadada ajitokeza kwenye maandamano akiwa na bango la kutafuta mume wa kumuoa

Wakati wenzake walijitokeza kwa wingi kuitaka serikali kupunguza gharama ya maisha, mwanamke huyo yeye aliweka wazi kwamba kilichomchukua kwenye maandamano ni kutafuta mume tu!

Muhtasari

• Kwa bahati nzuri, alikutana na mvulana ambaye pia alionekana kuwa na nia kama yake kwenye maandamano hayo.

• Katika video ya mtandaoni ya TikTok iliyooenezwa, kijana huyo, ambaye alikuwa amevalia nguo nyeusi, alionekana kwenye goti moja akiweka pete kwenye kidole chake.

Mrembo akitafuta mume na bango barabarani.
Mrembo akitafuta mume na bango barabarani.
Image: X, TikTok.

Huku mamia ya wananchi jijini Accra wakiwa wamejitokeza mitaani katika vuguvugu la maandamano kuishinikiza serikali kuwajibika, vuguvugur ambalo wamelipa jina kwa alama ya reli #OccupyJulorbiHouse, mwanadada mmoja amewashangaza watu kwa kujitokeza kwenye maandamano hayo akiwa na bango la kutafuta mume.

Maandamano hayo yameendelea kwa wiki ya pili sasa ambapo mamia ya watu wamejitoma mitaani wakishikiniza kuingia katika jumba hilo linalotoa huduma nyingi za serikali kuwasilisha malalamishi yao.

Kilichoshangaza wengi, wakati wenzake wanaandamana kuishinikiza serikali, mwanadada huyo alijitokeza na bango lenye ujumbe wa moja kwa moja akisema kwamba kwake yeye alijiunga na maandamano kutafuta mume tu wala si kivingine.

“As for me, I came to look for a husband (Kwangu mimi, nilikuja kutafuta mume)” Ujumbe huo ulisoma kwenye bango lake.

Katika habari inayofungamana na hiyo, kwenye picha zingine, Kwa bahati nzuri, kijana mmoja ambaye nia yake ya kujiunga na maandamano ilikuwa kuizomea serikali juu ya hali ngumu ya maisha nchini humo, alitumia fursa hiyo kukiri kumpenda mrembo huyo.

Katika video ya mtandaoni ya TikTok iliyooenezwa, kijana huyo, ambaye alikuwa amevalia nguo nyeusi, alionekana kwenye goti moja akiweka pete kwenye kidole chake.

Huku kukiwa na shangwe kutoka kwa watazamaji waliochangamka, mwanamke aliyejilegeza kwa haya alitabasamu huku mvulana akimvisha pete kidoleni.

 Kijana huyo kwa upande wake alisimama na kucheza kwa furaha huku akijua wazi kuwa anatoka kwenye maandamano akiwa mtu mwenye furaha.

Maandamano ya kulalamikia hali ngumu ya maisha yamekuwa yakikumba mataifa mengi ndani ya nje ya Afrika wananchi wakilia kupanda kwa gharama ya maisha na mfumuko wa kiuchumi.

Nchini Uingereza mwaka jana, mamia ya watu walijitokeza mitaani la kulemaza shughuli zote kutoka idara za afya, shule hadi biashara mitaani wakishinikiza serikali kuweka mpango madhubuti wa kuwalinda watumizi kutokana na hali mbaya ya uchumi.

Maandamano kama hayo pia yameshuhudiwa humu nchini mapema mwaka huu ambapo muunano wa upinzani uliwaongoza mamia ya wananchi kujitokeza mitaani katika maeneo mbali mbali wakiishinikiza serikali ya rais Ruto kufanya gharama ya maisha kuwa nafuu.