Samidoh hatimaye amposti Karen Nyamu, amsherehekea kimahaba na kuapa kutoficha mapenzi yao

"Sitacheza salama!" Samidoh alisema huku akibainisha wamba alikuwa tayari kutoficha mahusiano yao tena.

Muhtasari

•Samidoh alitumia wimbo wake ‘Mumbi’ kufufua kumbukumbu ya wakati uhusiano ulianzishwa, wakati mpenziwe alikuwa na haya sana akizungumza naye.

•Samidoh alimtambulisha Karen Nyamu kama ‘pacha’ wake na kukiri kwamba seneta huyo ndiye ‘scorpio’ anayempenda zaidi.

Seneta Nyamu na mpenzi wake Samidoh
Image: SAMIDOH// INSTAGRAM

Staa wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh mnamo Jumatatu jioni alimposti mpenzi wake Karen Nyamu na kumsherehekea vizuri kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mwimbaji huyo mashuhuri ambaye kwa muda mrefu amejaribu kuficha mahusiano hayo kutoka kwa umma aliamua kumsherehekea hadharani mama huyo wa watoto wake wawili mnamo siku yake maalum. Seneta huyo wa kuteuliwa wa UDA alikuwa anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Katika ujumbe wake kwa mpenziwe, Samidoh alimtambulisha kama ‘pacha’ wake na kukiri kwamba seneta huyo ndiye ‘scorpio’ anayempenda zaidi (mtu aliyezaliwa kati ya Oktoba na Novemba).

"Mtu tunayefanana, scorpio kipenzi," Samidoh aliandika kwenye picha yake na seneta Nyamu.

Mwimbaji huyo aliendelea kuweka wazi kwamba alikuwa tayari kutoficha uhusiano wao tena.

"Sitacheza salama. Heri ya kuzaliwa @senatorKarenNyamu,” aliandika.

Samidoh pia alitumia moja ya nyimbo zake za mapenzi kutuma ujumbe maalum kwa mama huyo wa watoto wake wawili.

Alitumia wimbo wake maarufu ‘Mumbi’ kufufua kumbukumbu ya wakati uhusiano wake ulipoanzishwa, wakati mpenziwe alikuwa na haya sana akizungumza naye. Katika wimbo huo, alibainisha kuwa hata wakati huo, angeona mustakabali machoni mwa mpenzi wake.

“Sijawahi kusahau nilipokuwa nikizungumza na wewe na ulikuwa unatengeneza michoro chini huku macho yako yakiwa yamejawa na aibu. Na nilipotazama machoni pako, ningeona mustakabali,” Samidoh alisema kwenye wimbo huo.

Chapisho la Samidoh la siku ya Jumatatu kumsherehekea mzazi mwenzake lilikuwa muhimu sana na la kipekee kwani ni nadra sana kwa mwanamuziki huyo mahiri kumpost seneta huyo au kuzungumza waziwazi kuhusu uhusiano wao hadharani.

Seneta Karen Nyamu aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa mnamo Jumatatu, Novemba 6, siku chache tu baada ya mpenzi wake Samidoh kusherehekea yake.

Mwimbaji huyo alifikisha umri wa miaka 33 mnamo Novemba 1, 2023 na Karen Nyamu akamfanyia karamu kubwa ya siku ya kuzaliwa siku moja baadaye.

Mama huyo wa watoto watatu alimfanyia Samidoh sherehe maalum ya siku ya kuzaliwa yenye mada ya soka. Karamu ilikuwa na keki ya siku ya kuzaliwa iliyopambwa kwa rangi za  buluu za klabu yake aipendayo ya kandanda, Chelsea.