Sonko akana kushiriki mapenzi na Karen Nyamu walipokutana, atoa ushahidi kuwa Samidoh alikuwepo

Mike Sonko alikanusha madai ya baadhi ya Wakenya kwamba walikutana kwa nia ya mapenzi.

Muhtasari

•Sonko alibainisha kuwa Samidoh pia alikuwepo wakati walipokutana, hivyo haingewezekana wao kulala pamoja kama ilivyodaiwa.

•Katika picha hiyo, wawili hao walionekana wenye furaha sana na hawakuwa na viatu kwenye miguu yao.

Image: TWITTER// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Mbuvi Sonko ameweka wazi kuwa hakushiriki mapenzi  na Seneta Karen Nyamu wakati wa mkutano wao wa Jumanne.

Katika taarifa yake Jumatano alasiri, mfanyibiashara huyo mbwenyenye alikanusha madai ya baadhi ya watumiaji wa mitandao kwamba walikutana kwa nia ya mapenzi.

Alibainisha kwamba mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, ambaye ni mpenzi wa Karen Nyamu pia alikuwepo wakati wa mkutano huo, hivyo basi haingewezekana wao kulala pamoja kama ilivyodaiwa.

"Wale wanasema ati jana nilikula senator, kwani siku hizi madem wanakula mbele za mabwana wao kama chakula," Mike Sonko alihoji kwenye Twitter.

Mwanasiasa huyo mwenye aliyezingirwa na utata aliambatanisha ujumbe wake na picha yake akiwa amesimama kati ya seneta Nyamu na mwimbaji huyo wa Mugithi.

Siku ya Jumanne, baadhi ya wanamitandao waliibua maswali kuhusu mkutano kati ya wanasiasa hao wawili baada ya Sonko kuchapisha picha yake na Karen Nyamu ndani ya afisi yake. Katika picha hiyo, wawili hao walionekana wenye furaha sana na hawakuwa na viatu kwenye miguu yao.

“Nomaree!” Sonko aliandika kwenye picha aliyoweka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Tazama maoni ya baadhi ya wanamtandao;-

Jaber is Jaber: Mhesh, uliskia mzee anaenda Haiti ukaona itakuwa wakati wako wa kung'aa.

Wangui Macharia: Mbona hamna viatu?

Indigochild: Hii imeenda.

Coastian_Icon: Ambieni Samidoh huu ni uzi wa usalama wa ndani maana sonkoree si mchezo.

Mike: "Yule ananipea, atakuletea.."

Mwaka uliopita, Sonko alifichua kwamba yeye ndiye aliyemuunganisha seneta Karen Nyamu na mwimbaji huyo wa Mugithi.

Gavana huyo wa zamani alidai kuwa  aliwaunganisha wazazi wenza hao katika hafla ya Mugithi Night iliyofanyika Dubai miaka kadhaa iliyopita. Sonko alikuwa akitoa maoni chini ya chapisho  la Nyamu kwenye Facebook wakati alipotoa ufichuzi huo.

"Mnafaa mniitie chai. Mimi ndio nilikupea Samidoh pale Dubai nikiwa na Moses Kuria wakati wa Mugithi night," alimwambia Karen.

Karen ambaye kwa sasa ana watoto wawili pamoja na Samidoh hakupinga kauli hiyo na badala yake akamuomba asifichue zaidi.

"Mdosi malizia tu hapo usitoe video," alimjibu Sonko.

Sonko anaonekana kuwa na uhusiano wa karibu sana na wazazi wenza hao wawili na mara kadhaa amekuwa akionekana nao.