Kimenukaa! Mama Dangote akosa kuyatambua kabisa mahusiano ya Diamond na Zuchu

“Hajawahi kuniletea Zuchu eti anataka kumuoa. Mimi Zuchu najua ni msanii wake,” Mama Dangote alisema

Muhtasari

•Mamake Diamond, Mama Dangote alibainisha kuwa bosi huyo wa WCB hajawahi kumtambulisha Zuchu kama mpenzi wake.

•Alisema Diamond amekuwa akihusishwa kimapenzi na wanawake wengi tangu aanze kazi yake ya muziki miaka mingi iliyopita.

hamtambui Zuchu kama mpenziwe Diamond.
Mama Dangote hamtambui Zuchu kama mpenziwe Diamond.
Image: HISANI

Mama ya mwimbaji wa bongo Diamond Platnumz, Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote amepuuzilia mbali tetesi kuwa mwanawe na Zuchu ni wapenzi.

Katika mahojiano na Wasafi Media, Mama Dangote alibainisha kuwa bosi huyo wa WCB hajawahi kumtambulisha Zuchu kama mpenzi wake.

Alibainisha kuwa anavyofahamu, binti huyo wa malkia wa taarab Khadija Kopa ni msanii tu chini ya lebo ya muziki ya Diamond Platnumz, Wasafi.

“Hajawahi kuniletea Zuchu eti anataka kumuoa. Mimi Zuchu najua ni msanii wake,” Mama Dangote alisema.

Mamake Diamond alibainisha kwamba mwanawe anaweza kuwa na uhusiano na wanawake hata mia moja huku akidai kwamba Mungu bado hajampa maagizo ya kuoa.

Aidha, alisema Zuchu si mwanamke wa kwanza kuhusishwa kimapenzi na mwanawe , akidai kuwa bosi huyo wa WCB amekuwa akihusishwa kimapenzi na wanawake wengi tangu aanze kazi yake ya muziki miaka mingi iliyopita.

"Mimi najua mchumba Yule aliyeleta mahari," alisema.

Jambo hilo limeendelea kuongeza sintofahamu kwa mashabiki ambao wana kila sababu ya kuamini kuwa mastaa hao wawili wa bongo fleva ni wapenzi. Kwa muda mrefu, waimbaji hao wawili wameonekana wakibarizi pamoja na kushiriki nyakati za kimapenzi kama vile kubusiana, kukumbatiana kimahaba na kupeana zawadi maalum.

Septemba mwaka jana, Tetesi za mzozo kati ya Mama Dangote na Zuchu ziliibuka baada ya mamake Diamond kudaiwa kum-unfollow binti huyo wa Khadija Kopa kwenye mtandao wa Instagram. Mama Dangote pia alidaiwa kukubaliana na maoni ya shabiki aliyependekeza Diamond kurudiana na Tanasha na kumtimua Zuchu.

Wakati akijibu tuhuma hizo, Mama Dangote aliweka wazi kuwa hajamfuata wala kum-unfollow mtu yeyote kwenye Instagram katika siku za hivi majuzi.

“Mimi wasije wakaniingiza kwenye mambo yao. Mimi sijamu-unfollow. Niliowa-follow hao hamsini, ndio hao hao hamsini. Sasa nimuunfollow kwa kipi?” Mama Dangote aliiambia Wasafi Media.

Aliongeza, “Mimi mwenyewe ata nikigombana na mtu atajua mwenyewe. Niliowa-follow ni hao hamsini ,sina hamsini na moja. Mambo ya kitoto ya zamani wasiniingize. Mimi najijua mtu mzima. Mimi nimuunfollow amenifanya nini?”

Mamake Diamond aliwasihi wanamitandao kuepuka kumuingiza kwenye ugomvi na Zuchu huku akimtaja malkia wa Zanzibar kama bintiye.

“Wasinigombanishe na mwanangu Zuchu. Mimi sina ugomvi na mtu. Wasiniingize kwenye mambo hayo,” alisema.