Mumewe Zari aachwa na machungu baada ya kuvamiwa na majambazi, kuibiwa vitu vya thamani

Shakib alikuwa kwenye duka kubwa karibu na nyumba yake mjini Kampala, Uganda aliposhambuliwa.

Muhtasari

•Mashahidi walimtambua mmoja wa wajambazi waliodaiwa kumwibia Shakib, ambaye anadaiwa kuwa mshirika wa mwanamuziki maarufu wa Uganda.

•Mfanyibiashara huyo aliapa kufanya uchunguzi zaidi ili kuhakikisha mhalifu anaadhibiwa.

Zari na mumewe Shakib
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mume wa mwanasosholaiti Zari Hassan, Shakib Cham Lutaaya mnamo siku ya Ijumaa jioni alivamiwa na majambazi na kuibiwa baadhi ya vitu vyake vya thamani.

Katika taarifa yake kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, mwanaume huyo wa miaka 31 alifichua kuwa majambazi waliomvamia walitoroka na simu zake mbili, cheni ghali na kiasi cha pesa ambacho hakijafichuliwa.

Alikuwa kwenye duka kubwa karibu na nyumba yake mjini Kampala, Uganda aliposhambuliwa.

“Wapendwa, niliibiwa saa kadhaa nyuma. Begi langu ambalo lilikuwa na simu zangu mbili, pesa taslimu na cheni za bei ghali zilinyakuliwa katika duka kubwa la mtaani kwangu,” Shakib alisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa jioni.

Aliendelea kufichua kuwa mashahidi waliweza kumtambua mmoja wa wajambazi waliodaiwa kumwibia, ambaye inasemekana ni mshirika wa mwanamuziki maarufu wa Uganda.

"Kumalizia hali hiyo ya jioni, watazamaji walinyoosha vidole kwa Benja fulani, anayedaiwa kuwa mshirika wa karibu wa msanii wa muziki Pallaso. Kwa heshima, nilimpigia simu Pallaso ambaye ni kama ndugu yangu. Hata hivyo, majibu yake hayakuwa ya kukatisha tamaa kwani alisema hamfahamu mtu kama huyo ninayemzungumzia. Alidai upuuzi, akionyesha tabia kwa kusisitiza hadhi yake ya supastaa ambaye anatembea na watu wengi,” Shakib alisema.

Hata hivyo, mfanyibiashara huyo aliapa kufanya uchunguzi zaidi ili kuhakikisha mhalifu anaadhibiwa.

"Nitabaki imara, naomba ushirikiano huku mimi na timu yangu tukilichunguza suala hili na naapa kumshughulikia Benja huyo na washirika wake," alisema.

Shakib Cham ambaye ni mume wa mwanasosholaiti na mfanyabiashara mashuhuri wa Uganda, Zari Hassan anaishi jijini Kampala, Uganda ambako anafanya biashara. Pia ana makazi nchini Afrika Kusini ambako mara nyingi huwa anakaa na mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz.