Baba wa kambo bora! Hisia nzuri huku Shakib akiboresha uhusiano na watoto wa Zari na Diamond

Mume huyo wa Zari mwenye umri wa miaka 31 alitumia muda mzuri na Tiffah na Nillan kwenye chumba cha mazoezi Jumamosi.

Muhtasari

•Shakib Lutaaya anaonekana kuendelea kujenga uhusiano mzuri na watoto wadogo wa mwanasosholaiti Zari Hassan.

•Shakib alionekana akiwasaidia watoto hao wa Diamond kufanya mazoezi kwa kutumia vifaa tofauti kwenye gym

akiwafunza Tiffah na Nillan
Shakib akiwafunza Tiffah na Nillan
Image: INSTAGRAM// SHAKIB CHAM

Mume wa Zari Hassan, Shakib Cham Lutaaya anaonekana kuendelea kujenga uhusiano mzuri na watoto wadogo wa mwanasosholaiti huyo wa Uganda.

Katika siku kadhaa za hivi majuzi, mfanyabiashara huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 31 amekuwa akitumia baadhi ya muda wake na watoto wadogo wa Zari, Tiffah Dangote na Prince Nillan. Wawili hao ni watoto wa mwanaosholaiti huyo na staa wa bongo fleva Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz.

Siku ya Jumamosi, Shakib alichapisha video nzuri zake na watoto hao wawili wadogo wakifurahia muda pamoja kwenye ukumbi wa mazoezi. Alionekana akiwasaidia watoto hao wa Diamond kufanya mazoezi kwa kutumia vifaa tofauti kwenye gym moja nchini Afrika Kusini ambako wanaishi.

Katika video za kwanza, mfanyibiashara huyo wa Uganda alionekana akiwainua Tiffah na Nillan hadi kufikia nguzo ambayo ilikuwa juu sana na kuwasaidia kufanya mazoezi. Baadaye aliwatazama wawili hao walipokuwa wakivuta kamba nzito ya mazoezi kabla ya kuwapa mafunzo ya ndondi.

"Wakati wa kusonga," Shakib alisema chini ya video iliyomuonyesha akiwafundisha watoto hao wawili mitindo ya ndondi.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya muungano mzuri kati ya mume huyo wa Zari na bintiye Diamond, Tiffah Dangote kuonekana wazi.

Wiki jana, Zari alishiriki video nzuri ya mume wake Shakib akikaribishwa nyumbani na binti yake Tiffah  kwa njia ya kupendeza sana. 

Katika video hiyo ambayo Zari alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Tiffah ambaye ni mtoto wa kwanza wa mwanasosholaiti huyo na Diamond Platnumz alionekana akimkimbilia Shakib alipokuwa akishuka kwenye gari lake.  

Punde baada ya malkia huyo wa miaka minane kufika pale alipokuwa Shakib, babake huyo wa kambo alimkumbatia vizuri na kumuinua kwa mikono miwili. Wawili hao kisha walionekana kuwa na mazungumzo mafupi nje ya gari.

Zari alionekana kufurahishwa sana na uhusiano mzuri ulioonyeshwa kati ya mumewe huyo mwenye umri wa miaka 32 na bintiye. Aliambatanisha video yake na wimbo “I love you baby” wa Emilee.

Hii sio mara ya kwanza kwa uhusiano mzuri kati ya Shakib na Tiffah kuonekana wazi. Wawili hao wameonekana kuhusiana vizuri katika siku za nyuma.