Ndoa ya Guardian Angel yabarakiwa baada ya Esther Musila kumpeleka kukutana na familia yake

Miongoni mwa watu ambao wanandoa hao walikutana nao ni shangazi zake Esther Musila, mjomba wake na kaka yake.

Muhtasari

•Bi Musila alimpeleka Guardian Angel nyumbani kwao kijijini kukutana na familia yake ya upande wa mamake na kupokea baraka.

•Musila alifichua kwa nini mjomba wake hakuhudhuria harusi yao miaka miwili iliyopita akisema alikuwa nje ya nchi wakati huo.

 

alimpeleka Guardian Angel kukutana na wanafamilia wake.
Esther Musila alimpeleka Guardian Angel kukutana na wanafamilia wake.
Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Mke wa msanii Guardian Angel, Bi Esther Ngenyi Musila, mnamo siku ya Ijumaa alimpeleka mwimbaji huyo wa nyimbo za injili nyumbani kwao kijijini ili kukutana na familia yake ya upande wa mamake na kupokea baraka.

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alifichua habari hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alionyesha baadhi ya picha zilizopigwa wakati wa mkutano kati ya pande hizo mbili.

Miongoni mwa watu ambao wanandoa hao walikutana nao ni shangazi zake Esther Musila, mjomba wake na kaka yake.

"Ndugu yangu Fred, mimi na mume wangu tulipokea baraka zetu kutoka kwa mjomba na shangazi zetu wapendwa," Esther Musila alisema chini ya picha alizochapisha siku ya Jumamosi.

 Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alisherehekea kupata baraka kutoka kwa kaka pekee wa mama yake aliye hai ambaye alimtaja kuwa msomi mashuhuri.

Musila aliendelea kufichua ni kwa nini mjomba huyo wake hakuhudhuria harusi yao nzuri miaka miwili iliyopita akisema kwamba alikuwa nje ya nchi wakati huo.

"Jana (Ijumaa), tulitimiza, kulipa deni letu, na kupata baraka za kaka wa pekee wa mama yangu mjomba David Kivuva, msomi mashuhuri, kwa kushiriki keki," Esther Musila alisema.

 Aliongeza, "Hakuweza kuhudhuria harusi yetu kwani alikuwa akiwatembelea watoto wake nje ya nchi wakati huo."

Bi Musila pia alichukua fursa hiyo kusherehekea dada pekee wa mamake aliye hai ambaye alifichua kuwa ana umri wa miaka 85.

"Dada pekee wa mama yangu aliye hai Aunt Kavindu ambaye ana umri wa miaka 85.. vinasaba vikali," alisema.

Esther Musila ambaye amempiku umri Guardian Angel kwa takriban miongo miwili alifunga pingu za maisha na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili mwanzoni mwa mwaka wa 2022 na wawili hao wamekuwa wakiishi pamoja kwa furaha. Hata hivyo, si kila mtu anafurahia ndoa yao kwani baadhi ya Wakenya wamekuwa wakikosoa muungano wao na kumkosoa mama huyo wa watoto watatu kwa kuolewa na mwanamume ambaye ni mdogo zaidi yake.

Bi Musila hata hivyo ameendelea kuwasuta watu wanaopinga  ndoa yao na wale wanaowakosoa kuhusiana na tofauti kubwa ya umri kati yao.