Diamond ashindwa kuvumilia upweke baada ya kuachwa, atua nyumbani kwa kina Zuchu kuomba msamaha

Alisema hatua hiyo ya kuomba radhi huenda ikamfanya binti huyo wa Khadija Kopa kutulia na kurudiana naye.

Muhtasari

•Diamond alitangaza kuwa yuko njiani kuelekea nyumbani kwa kina Zuchu kuomba radhi baada ya kushauriwa kuchukua hatua hiyo muhimu.

•Hatua hii imekuja saa chache tu baada ya Zuchu kutangaza mwisho wa uhusiano wao wa kimapenzi 

ZUCHU NA DIAMOND PLATNUMZ
Image: WASAFI/INSTAGRAM

Bosi wa WCB Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amedokeza kuhusu kumuomba msamaha mpenzi wake Zuchu ambaye alitangaza amemuacha siku ya Ijumaa.

Katika taarifa yake ya Jumamosi mchana, staa huyo wa bongo fleva alitangaza kuwa yuko njiani kuelekea nyumbani kwa kina Zuchu Zanzibar kuomba radhi baada ya kushauriwa kuchukua hatua hiyo muhimu.

Alisema hatua hiyo ya kuomba radhi huenda ikamfanya binti huyo wa Khadija Kopa kutulia na kurudiana naye.

“Kaka yangu @hajismanara jana alinishauri niache kiburi niende Zanzibar nikaombe Msamaha pengine nitaweza Rudiwa, Baada Kum’bishia kwa Muda Mrefu nikagundua Yuko sahihi,” Diamond alitangaza kupitia Instagram.

Aliongeza, “Nami niko njiani kuelekea Zanzibar kuelitekeleza hili. Nahitaji sana mawazo yenu kwenye Ubunifu wa Kuomba Msamaha, lakini pia Uwepo wenu kwenye Full Moon Party Kendwa Rocks Zanzibar leo ili kunisaidia kulikamisha hili.”

Hatua hii imekuja saa chache tu baada ya Zuchu kutangaza mwisho wa uhusiano wao wa kimapenzi uliodumu kwa takriban miaka miwili.

Katika taarifa yake Ijumaa jioni, malkia huyo wa bongofleva alikiri kuwa kwa muda mrefu amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na bosi wake.

Hata hivyo, alifichua kuwa uhusiano huo uliozungumiwa sana kote barani Afrika umefikia kikomo akidokeza kuwa Diamond amemkosea heshima.

“HABARI FAMILIA .ILIBIDI KUPOST HII ILI KUFUTA DHAMIRI YANGU. KUANZIA LEO HII MIMI NA NASIBU (DIAMOND) HATUKO PAMOJA,” Zuchu alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, “NAJUA HILI LIMEKUWA JAMBO LETU LAKINI AS HARD AS IT IS KUMUACHA MTU UNAEMPENDA HII NAOMBA MUNGU IWE YA MWISHO NA NIANZE MAISHA MAPYA. MAPENZI NI HESHIMA KWA BAHATI MBAYA SANA HIKO KIMEKOSEKANA KWETU.”

Licha ya kusambaratika kwa uhusiano wao wa kimapenzi, Zuchu hata hivyo aliweka wazi kuwa wataendelea kufanya kazi pamoja katika WCB.

Binti huyo wa Khadija Kopa alitangaza kuwa sasa yuko single akibainisha wazi kuwa yuko tayari kwa sura mpya ya maisha yake kama mtu huru.

“NAMTAKIA YEYE NA FAMILIA YAKE KILA LA KHERI KABISA .TUMEISHI VIZURI LAKINI NADHANI HII SIO RIZKI .MWAKA HUU NIMEJIFUNZA KUSEMA HAPANA KWA KILA KITU KISICHONIPA FURAHA AMA BAADA YA KUSEMA HAYA NAONA KABNYE MASHAURI YA KUFURAHIA NA KUFURAHIA MPAKA . . KWA SASA KAZI IENDELEE NA MIMI NIKO SINGLE ���.,” Zuchu alisema.

Tangazo hili limekuja saa chache baada ya Diamond Platnumz kuonekana akiwa ameshikana mikono kimahaba na mzazi mwenzake Zari Hassan.