Harmonize awatupia vijembe Diamond na Alikiba huku akitangaza taaluma yake mpya

Konde Boy amedai kwamba ushindani katika tasnia ya bongo fleva sasa umetoka kwenye muziki hadi kwenye media.

Muhtasari

•Harmonize ameonekana kuibua mashambulizi mapya dhidi ya Diamond Platnumz na Alikiba huku akitoa tangazo kubwa taaluma yake.

•Alijivunia kuwa hodari sana katika ndondi na hata akataka kuvishwa pete na bondia wa kulipwa.

Diamond Platnumz, Harmonize, Alikiba
Image: INSTAGRAM

Bosi wa Konde Music Worldwide Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameonekana kuibua mashambulizi mapya dhidi ya wasanii wenzake wa bongofleva Diamond Platnumz na Alikiba huku akitoa tangazo kubwa taaluma yake.

Katika chapisho la Jumanne asubuhi, mwimbaji  huyo wa kibao ‘Single Again’ alionekana kuwashambulia waimbaji hao wawili kuhusu vyumba vyao vya habari.

Alidai kwamba ushindani katika tasnia ya bongo fleva sasa umetoka kwenye muziki hadi kwenye media.

“Ushindani kwenye Muziki umepungua sanaa!!!! Nguvu Nyingi zimehamia kwenye media !!!” Harmonize aliandika Jumanne asubuhi.

Aliambatanisha kauli yake na video na picha zake akiwa amevalia mavazi ya ndondi na kudokeza kuwa ni mchezo ambao pia anaujua vizuri.

Alijivunia kuwa hodari sana katika ndondi na hata akataka kuvishwa pete na bondia wa kulipwa.

"Nadhani ni wakati wa Aiii ⏰ Kuonyesha Ulimwengu 🌎 Sehemu Nyingine ya Wanaume !!! Mchezo Mwingine Ambao Naweza Kucheza Kweli 🥊🥊 Tag Mpiganaji Uliyempenda Zaidi Aliyeshinda angalau mkanda mmoja 🥋!!! Tafadhali Namaanisha PROFESSIONAL WITH 🥋 sitaki Kesiiii 🙏 .” alisema.

Aliongeza, "Tufanye RAUNDI SITA Baada ya RAMADHANI na 100k USD 💰💰 kama kweli unaweza kupambana ANZA SASA CHANGIA HIZO PESA Coz After RAMADHAN im Drop GLOBAL ALBUM 💿 sitokuwa Na TIME KABISAA!!!!!"

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mwimbaji Alikiba kuzindua Crown Media kuungana na Diamond Platnumz katika orodha ya mastaa wa bongofleva wanaomiliki vyombo vya habari,

Alikiba alizindua vituo vyake vya media, Crown FM na Crown TV mapema mwezi huu wakati akisherehekea miaka ishirini katika tasnia ya burudani.

Huku akizungumzia sababu ya kuamua kuzindua vituo vyake vya habari, staa huyo wa bongo fleva alibainisha kuwa redio na tv zimekuwa nguzo kuu katika kujenga taaluma yake ya muziki.

“Media ni chombo chenye nguvu sana, Media ndio iliyonifanya kuwa Alikiba huyu wa leo,” Alikiba alisema wakati wa uzinduzi wa vituo vyake.

Aliongeza, “Ila pia mimi nilikuwa silali bila redio yangu ndogo niliyoletewa zawadi na baba yangu kupigwa muziki. Changamoto nilizopitia na kutatua kuleta suluhisho kwenye media ndivyo ndivyo vimenipa msukumo."