Bahati na Diana Marua wapingana vikali kuhusu kupata mtoto mwingine

Wanandoa hao ambao tayari wana watoto watatu pamoja kisha walijibizana vikali kuhusu suala la kuongeza mtoto wa nne.

Muhtasari
  • Bahati aliweka wazi kuwa bado hajaridhika na watoto wanne ambao tayari anao.
  • Kwa upande wake, Diana Marua aliweka wazi kuwa hana nia ya kupata mtoto wa nne.
Image: YOUTUBE// DIANA MARUA

Wanandoa mashuhuri wa Kenya, Kelvin ‘Bahati’ Kioko na mkewe Diana Marua wamefunguka kuhusu suala la kupata mtoto mwingine.

Wanandoa hao walitumia chaneli ya YouTube ya Diana Marua kujibu maswali yaliyoulizwa na mashabiki wao, ambapo walishiriki majibu yanayokinzana kuhusu kupata mtoto wa nne pamoja.

“Mna mpango wa kupata mtoto mwingine?” shabiki aliuliza.

Bahati aliweka wazi kuwa bado hajaridhika na watoto wanne ambao tayari anao.

“Bila shaka mimi bado nataka watoto zaidi. Kwa hivyo ninapanga kupata zaidi,” mwimbaji huyo alisema.

Kwa upande wake, Diana Marua aliweka wazi kuwa hana nia ya kupata mtoto wa nne.

“Mwisho wa siku mimi ndiye nambeba mtoto. Kwa hivyo, sina mpango wa kupata mtoto mwingine,” Diana Marua alisema.

Aliongeza, “Unataka kupata watoto wengine, nani atawabeba? Wewe ndiye utawabeba?”

Bahati alimjibu mkewe, "Tayari nimezibeba hapa (akionyesha sehemu zake za uzazi)"

Wanandoa hao ambao tayari wana watoto watatu pamoja kisha walianza kujibizana vikali;

Bahati: Tumbo ni kitu cha kunyimana?

Diana Marua: Tumbo kwa miezi tisa nikisumbuana na morning sickness wewe uko huko unapata raha, uko huko unajibamba. Ati nikose kula kitu nataka juu ya morning sickness?

Bahati: Mawe huwa hukuli? Si hiyo ndo huwa unapenda? Hutaki kokoto? Si hiyo ndo kitu huwa unapenda.

Diana: Mimi nikule mchanga, unataka kunirudisha hapo?Na kokoto na mawe?

Bahati: Nishawahi kunyima mchanga? Nishawahi kunyima mawe? Nishawahi kunyima ile mchanga ni kama imenyeshewa na mvua?

Diana: Mimi nikae ati sasa nakula tu Githeri imechanganywa na parachichi imeturn imekuwa green, hiyo tu ndo nakula? Na juisi ya apple? Hiyo tu ndo nitakuwa nakula maisha yangu yote? Sifanyi!!

Bahati: Mimi ujue napanga kupata watoto zaidi.

Diana: Haya, utaniambia na nani!

Bahati tayari ni baba mzazi wa watoto wanne na anamlea mvulana mwingine mmoja. Msanii huyo ana watoto watatu na mkewe Diana Marua na binti mwingine na mpenzi wake wa zamani Yvette Obura.

Kwa upande wake, Diana Marua ana watoto watatu tu ambao alipata na mwimbaji.