•Mercy Kyallo alijitolea kuwasaidia wanawake ambao hawana uwezo wa kuzaa wa kufanyiwa utaratibu wa Vitro fertilization (IVF) akiwa na umri wa miaka 18.
•Utaratibu huo uliweza kuzaa matunda licha ya changamoto kwani hatimaye madaktari walifanikiwa kutoa mayai kutoka mwili wake.
Mfanyibiashara Mercy Kyallo amefunguka kuhusu wakati ambapo utaratibu wa kutoa mayai mwilini wake ilimwendea vibaya.
Akiwa bado na umri mdogo wa miaka 18, dada huyo mdogo wa mtangazaji Betty Kyallo alijitolea kuwasaidia wanawake ambao hawana uwezo wa kuzaa wa kuchukua hatua ya kufanyiwa utaratibu wa Vitro fertilization (IVF) .
IVF ni utaratibu halali wa kimatibabu ambapo yai hutolewa kutoka kwa mwili wa mwanamke na kurutubishwa na mbegu za kiume nje ya mwili.
Mercy hata hivyo alikumbwa na matatizo chungu nzima mwili wakati akifanyiwa utaratibu huo kwani mwili wake haukupokea dawa.
"Mambo yaliharibika. Haikufaa yaharibik na madaktari waliokuwa wanafanya utaratibu huo sio watu wabaya lakini mwili wangu haukuwa unakubali dawa. Nilikaribia kupoteza maisha yangu," Mercy alisema katika mahojiano na Mpasho.
Mfanyibiashara huyo alifichua kuwa utaratibu huo hata hivyo uliweza kuzaa matunda licha ya changamoto kwani hatimaye madaktari walifanikiwa kutoa mayai kutoka mwili wake.
Alisema alijitolea kufanyiwa utaratibu huo baada ya kugundua shida ambazo wanandoa wasioweza kupata watoto hukumbana nazo.
"Nilitaka sana kusaidia, hata napenda jambo hilo. Lakini labda wanawake wengine si wazuri kufanyiwa utaratibu huo. Wanawake wengine hawawezi kutoa yai na mimi ni mmoja wao," Alisema.
Licha ya kuwa mayai yalitolewa kutoka kwa mwili wake, Mercy hata hivyo hafahamu ikiwa yalitumika kutengeneza watoto.
"Baada ya kutoa mayai huwa hujui chochote baada ya hapo," Alisema
Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 29 pia aliweka wazi kuwa anapanga kupata watoto wake katika siku za usoni.
Alidokeza kuwa tayari amepata mchumba ambaye ananuwia kupata watoto naye.
"Nimekuwa mwenye bidii na maono, ni wakati wa ukurasa mwingine wa maisha yangu. Nina furaha," Alisema.
Hivi majuzi Mercy na dada zake wawili Betty na Gloria Kyallo walizindua Reality Show yao inayotambulika kama 'Kyalo Kulture' ambapo watakuwa wanafichua mambo mengi kuhusu maisha yao.