"Kutafuta mapenzi," Betty Kyalo azungumzia maazimio yake anapotimiza miaka 33

Muhtasari

•Betty alisema anakusudia kuendelea kufurahia maisha, kutengeneza pesa zaidi na kutafuta mapenzi.

Image: INSTAGRAM// BETTY KYALLO

Usiku wa Alhamisi mtangazaji na mfanyibiashara mashuhuri Betty Kyalo aliandaa karamu kubwa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Mama huyo wa binti mmoja alisherehekea siku hiyo maalum kwake na marafiki zake na baadhi ya wanafamilia.

Mmoja wa waliohudhuria karamu ya Betty ambayo iliandaliwa Club Gemini ni dadake Mercy Kyallo. Mercy alitumia fursa hiyo kumuuliza dadake kuhusu maazimio yake katika kipindi cha mwaka moja kiijacho.

"Kwa hivyo unahitimu miaka 33, una yepi ya kusema," Mercy Kyallo alimuuliza dadake.

Betty alisema anakusudia kuendelea kufurahia maisha, kutengeneza pesa zaidi na kutafuta mapenzi.

"Nitaendelea kula maisha kwa kijiko kikubwa, kutengeneza pesa  mingi na kutafuta mapenzi," Betty alisema.

Mercy alimtakia dadake mafanikio katika maazimio hayo yake hasa katika azimio la kutafuta mapenzi. "Natumai utayapata,"

Betty Kyallo na dadake Mercy Kyallo
Betty Kyallo na dadake Mercy Kyallo
Image: INSTAGRAM// BETTY KYALLO

Matamshi haya yanajiri miezi michache tu baada ya mtangazaji huyo kutengana na mpenzi wake wa muda mfupi Nick Ndeda.

Hivi majuzi Betty aliweka wazi kuwa mahusiano yake na wakili huyo yalikabiliwa na changamoto na wakaafikia kutengana.

Hapo awali, mtangazaji huyo alikuwa amedai kwamba mwaka huu anakusudia kuangazia biashara zake na malezi ya bintiye Ivanna.

"Kwa sasa, mimi niko sawa. Mwaka huu ninatimiza miaka 33 kama Yesu na ninataka kuhakikisha kwamba ninatimiza ndoto zangu zote. Nia yangu ni biashara na kutafuta pesa za binti yangu." Betty alisema akiwa kwenye mahojiano na Plug TV.

Betty atakuwa anafikisha miaka 33 mnamo Machi 15.