Diamond asafirisha familia, wandani, washirika na Watanzania wengine sita hadi Qatar (+video)

Diamond alikiri kuwa na hamu kubwa ya kushuhudia Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Muhtasari

•Diamond alisafiri kwa ndege kutoka Tanzania hadi nchi hiyo ndogo ya Asia siku ya Jumatatu na aliandamana na kundi la wanafamilia,  marafiki na baadhi ya washirika wake.

•"Natamani kuona Brazil, Natamani nitazame Argentina nikamuone Messi. Pia natamani nimuone Mbappe," alisema.

Diamond Platnumz
Image: Diamond Platnumz Instagram

Staa wa Bongo Diamond Platnumz yupo nchini Qatar kwa ajili ya kushuhudia moja kwa moja mechi za Kombe la Dunia.

Diamond alisafiri kwa ndege kutoka Tanzania hadi nchi hiyo ndogo ya Asia siku ya Jumatatu na aliandamana na kundi la wanafamilia,  marafiki na baadhi ya washirika wake.

Picha na video za safari hiyo zilichapishwa kwenye  ukurasa rasmi wa lebo ya WCB.

"Timu ya ushindi njiani kuelekea Qatar #Qatar2022 #FIFAWORLDCUP," taarifa iliyondakiwa chini ya video ya wasafiri walioandamana na Diamond ambayo ilichapishwa kwenye ukurasa wa Instagram wa WCB ilisoma.

Miongoni mwa walioandamana na bosi huyo wa WCB katika safari hiyo ni pamoja na Mama Dangote na mpenzi wake Uncle Shamte, Esma Platnumz, Mbosso, meneja Ricardo Momo, msemaji wa Yanga S.C Haji Manara, Baba Levo, Mwijaku pamoja na mlinzi rasmi wa Diamond Onesmo Amos.

Kabla ya kuabiri ndege, Diamond alisema kwamba alikuwa na hamu kubwa ya kusafiri hadi Qatar kushuhudia moja kwa moja michuano ya Kombe la Dunia kwa mara yake ya kwanza.

"Natamani kuona Brazil, Natamani nitazame Argentina nikamuone Messi. Pia natamani nimuone Mbappe," alisema.

Mwijaku ambaye hapo awali alikuwa chawa wa bosi wa Konde Music Worldwide Harmonize kabla ya kumtema na kuungana na Diamond alionekena kuifurahia sana safari hiyo kwa kuwa walikaa sehemu ya VIP.

"Huduma za VVIP, matajiri tumeingia DOHA kwa hisani ya Wasafibet," aliandika chini ya video iliyoonyesha akiwa ndani ya ndege.

Pamoja nao katika ndege hiyo walikuwepo Watanzania wengine sita waliofadhiliwa na Wasafi Bet yake Diamond Platnumz.