Harmonize hatimaye afunguka kuhusu sababu ya kutengana na Kajala

Alidokeza kuwa mahusiano yalisambaratika baada ya kumpata mpenziwe ametumiwa meseji na mwanamume mwingine.

Muhtasari

•Katika video hiyo, wawili hao walijadili kuhusu Harmonize kutengana na mpenzi wake ambaye hakutambulishwa.

•Bosi huyo wa Kondegang alibainisha kwamba alisikitika sana kutokana na tukio hilo kiasi cha kukata tamaa na mapenzi.

Harmonize na mchumba wake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Siku ya Jumanne, mwimbaji wa bongo Harmonize aliachia video fupi ya mazungumzo yake na mtayarishaji Director Kenny ambayo ilirekodiwa wakati walipokuwa wakirekodi video ya wimbo wa ‘Single Again’.

Katika video hiyo, wawili hao walijadili kuhusu Harmonize kutengana na mpenzi wake ambaye hakutambulishwa. Alidokeza kuwa mahusiano yalisambaratika baada ya kumpata mpenziwe ametumiwa meseji na mwanamume mwingine.

“Nilikuta meseji kwenye simu yake, mwanaume akiwa amemtumia meseji. Alianza kuniripukia kana kwamba anataka kupigana na mimi, nikamwambia sitaki kupigana naye, huwa sipigani na wanawake. Nilimwambia achukue simu yake," Konde Boy alimhadithia Director Kenny kwenye video iliyochapishwa YouTube.

Bosi huyo wa Kondegang alibainisha kwamba alisikitika sana kutokana na tukio hilo kiasi cha kukata tamaa na mapenzi.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa video hiyo ni sanaa tu na mazungumzo yake na Kenny hayakuwa  kuhusu sababu halisi ya yeye kuachana na muigizaji Frida Kajala Masanja mwishoni mwa mwaka jana.

 "Stori iliyo ndanio haihusiani kabisa na uhalisia wa maisha yangu. Stori imetunga na kuongozwa na Director Kenny. Aliwaza nini?? Sijuwi kiukweli," alisema.

Mwimbaji huyo aliendelea kufichua kwamba hajawahi kushiriki na mtu yeyote ukweli wa yeye kutengana na muigizaji huyo.

"Sijawahi kumhadithia yeyote kuhusu kilichofanyika!! Kifupi sikutaka hata ushauri  wowote. Ila siku nikilewa uuwi," alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja kuweka mambo wazi kuhusu kilichowatenganisha.

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha hapa nchini, Kajala alidokeza kuwa alimtema Harmonize kwa sababu ya mazoea.

"Sijui niseme nini. Labda mazoea. Mtu akishakuzoea sana anakuchukulia poa," alisema.

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alidokeza kwamba Harmonize bado hakuwa tayari wakati alipoamua kutulia naye kwenye mahusiano na kuwa huenda alihitaji nafasi ya kufanya mambo yake binafsi.

"Yaani mimi hata simlaumu, kwa sababu yeye ni kijana mdogo. Labda alihitaji nafasi, tulikuwa tuko karibu sana.

Yeye mara ya kwanza nahisi labda aliona kama mzaha akisema nataka huyu mtu, nataka niwe naye 24/7.  Mnaamka wote mnaenda gym, mnafanya hiki na kile. Labda alikuwa anahitaji nafasi yake afanye vitu vyake," alisema.

Kajala alibainisha kwamba alikubali kurudaina na bosi huyo wa Konde Music Worldwide kwa kuwa bado alikuwa anampenda.

Hata hivyo, alifichua kuwa tayari alikuwa amesonga mbele na maisha yake kabla ya Konde Boy kunyeyekea na kuomba radhi.

"Nilirudiana naye kwa sababu nilikuwa nampenda. Nilimove on, lakini ilikuwa mtu ambaye bado yupo. Alafu alipoomba msamaha nilijua.. sijui niseme nini," muigizaji huyo alisema kabla ya kukosa maneno ya kuelezea.

Mama huyo wa binti mmoja alikiri kwamba Harmonize alifanya wimbo 'Nitaubeba' maalum kwa ajili yake. Aliendelea kusifia kipaji cha mpenzi huyo wake wa zamani huku akitaja nyimbo zake kuwa nzuri.