Hii imeenda! Mzazi Mwenza wa Harmonize, Mama Zuuh Konde aolewa

Shanteel alionekana mwenye bashasha tele na aliyefurahishwa na hatua yake mpya.

Muhtasari

•Taarifa kutoka Tanzania zinaashiria kuwa mama huyo wa binti mmoja alifunga pingu za maisha na mchumba wake visiwani Zanzibar siku ya Ijumaa.

•Watu wake kadhaa wa karibu walimsherehekea na kumpongeza kwa kupiga hatua ya ndoa.

ameolewa
Mzazi Mwenza wa Harmonize, Official Shanteel ameolewa
Image: HISANI

Mzazi mwenza wa staa wa Bongo Harmonize, Official Shanteel almaarufu Mama Zuuh Konde hayupo sokoni tena.

Taarifa kutoka Tanzania zinaashiria kuwa mama huyo wa binti mmoja alifunga pingu za maisha na mchumba wake visiwani Zanzibar siku ya Ijumaa. Walakini, kuna maelezo machache sana kumhusu mumewe.

Video na picha za harusi hiyo zilizofikia Radio Jambo zilimuonyesha Mama Zuuh aliyepambwa vizuri akiwa amevalia gauni la rangi ya bluu lenye mapambo mbalimbali ya kuvutia huku akisherehekea siku hiyo yake kuu. Alionekana mwenye bashasha tele na aliyefurahishwa na hatua yake mpya.

Watu wake kadhaa wa karibu walimsherehekea na kumpongeza kwa kupiga hatua ya ndoa. 

"Hongera dada yetu mkubwa @official_shanteel," qu33n_sr alimwambia.

Fettyfinenyashi alimwambia, "Mashallah @official_shanteel. Hongera sana sanaa."

Mapema mwaka huu, Harmonize alimlimbikizia sifa kemkem mzazi huyo mwenzake baada ya kutumia ukurasa wa binti yao, Zuuh Konde kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

Mwezi Machi,  Shanteel aliandika ujumbe mzuri wa siku ya kuzaliwa kwa mwimbaji huyo kwa niaba ya binti yake. Katika ujumbe huo, Zuuh alitambua uwepo wa babake katika maisha yake na muungano wao mzuri.

"Kheri ya Siku ya Kuzaliwa Baba! Shukran kwa kila kitu ulichonipa. Kila siku uko kwa ajili yangu baba na rafiki bora pia. Hakuna muungano mwingine kama wetu. Nakupenda baba @harmonize_tz," ujumbe ulisomeka. 

Konde Boy alibainisha kuwa alitambua mzazi mwenzake ndiye aliyemwandikia binti yao ujumbe huo na hivyo kutoa shukrani kwake.

"Mama Zurekha asante kwa kugusa maisha yangu. Najua Zuu hawezi kuandika haya yote ila  hii ina maana kubwa sana kwangu." alisema.

Wakati huohuo, bosi huyo wa Kondegang alidokeza kuwa mzazi huyo mwenzake amekuwa akitamani wawe pamoja. Pia aliweka wazi kuwa kamwe huwa hachukulii upendo wa Shanteel kuwa za kawaida tu.

 "Zuuh akishakuwa mkubwa ataona na kujua kwa kiasi  gani ulitamani wazazi wake tuwe pamoja!!!  Ingawa ukipanga na Mungu Mtukufu anapanga. Kama ilivyo wazi, hatujawahi kwa wapenzi kiivyo lakini nakuahidi maisha yamenifundisha kukuona wa thamani na nastahili kubadilisha maisha yako kama ulivyofanya niitwe baba,"

Kufuatia hayo, Kondeboy  aliahidi kumtuza mzazi huyo mwenzake kwa gari, nyumba na biashara katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

"Huwezi zaa na Konde ukawa unatia huruma. Hata nisipokuwa na Hela watu wananipenda saana siwezi shindwa vitu vidogo," alisema.

Ingawa haijulikani kabisa kama waliwahi kuchumbiana rasmi, Harmonize na Official Shanteel walishiriki kitu pamoja ambacho kilipelekea kuzaliwa kwa binti yao mrembo,  Zuuh Konde mwaka wa  2019. Zuuh ni mtoto wa pekee wa mwanamuziki huyo wa Bongo ambaye anajulikana.