Baby Mama wa Harmonize afunguka kurudiana na kuolewa naye baada ya "kumaliza mizunguko"

"Mpaka amalize mizunguko yake mie nitakuwa nishaolewa," alisema.

Muhtasari

•Shanteel alifichua kwamba bado huwa anawasiliana na mzazi mwenza huyo wake kuhusu masuala ya malezi ya binti yao.

•Pia alibainisha kwamba yuko na mtoto mmoja tu, Zuuh Konde ambaye alipata na Harmonize miaka kadhaa iliyopita.

Official Shanteel na Harmonize
Image: INSTAGRAM

Huku vita vya maneno makali baina ya Harmonize na Rayvanny vikiendelea kwenye Instagram siku ya Jumatatu, mzazi mwenza wa bosi huyo wa Kondegang, Official Shanteel aliwashirikisha mashabiki wake kwenye kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao huo.

Katika kipindi hicho, wanamitandao walimuuliza mamake Zuuh Konde maswali mbalimbali ya kibinafsi, ya kimaisha na ya kikazi yakiwemo kuhusu uhusiano wake na Harmonize.

Mmoja wa wafuasi wake alimuuliza kwanini alikubali kupata mtoto na staa huyo wa Bongo ilhali hawakuwa kwenye ndoa halisi. 

"Kwani kuzaa na mtu lazima muwe wanandoa," alijibu.

Shanteel alifichua kwamba bado huwa anawasiliana na mzazi mwenza huyo wake kuhusu masuala ya malezi ya binti yao.

Shabiki wake mwingine alitaka kujua kama anaweza kukubali kuolewa na Harmonize mara tu atakapomaliza kujifurahisha na wanawake wengine.

"Mpaka amalize mizunguko yake mie nitakuwa nishaolewa," alisema.

Pia alibainisha kwamba yuko na mtoto mmoja tu, Zuuh Konde ambaye alipata na Harmonize miaka kadhaa iliyopita.

Official Shanteel alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Harmonize wakati mwanamuziki huyo alikuwa bado akichumbiana na Sarah Michelloti. Uhusiano huo wa kipindi kifupi ulifanya wawili hao kujaliwa mtoto mmoja  wa kike pamoja, Zulekha Nasra (Zuuh Konde) na pia ulivunja ndoa ya bosi huyo wa Kondegang na Sarah.

Mwaka wa 2021, Harmonize alipokuwa akizindua albamu yake  'High School' alifunguka kuhusu utata uliozingira kuzaliwa kwa bintiye.

Mwimbaji huyo alifichua kwamba kuzaliwa kwa mtoto huyo ndicho chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake ya kwanza na Sarah Michelloti.

Harmonize alisema ndoa yao ya miaka minne ilianza kusambaratika wakati mpenzi wake alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto.

"Ilikuja kipindi akawa anasafiri kuenda kwao. Nilikuwa Tanzania na kama unavyojua umbali wa mapenzi unapokuwa nikaishia kutembea na mwanamke ni mama Zuuh sasa hivi. Kwa mipango ya mwenyezi Mungu nikamfanya mjamzito." Harmonize alisema.

Konde Boy alifichua kwamba Shanteel alikuwa na wasiwasi kuhusu ujauzito huo na hata alikuwa tayari kuutoa ila akamkataza.

Alisema kuwa alikubali majukumu na akahudumia ujauzito ujauzito hadi mtoto alipozaliwa.

"Akaniambia na kuniuliza ikiwa niko tayari ama atoe. Kwa kuwa mimi ni Muislamu, kutoa mimba ni kushiriki  dhambi.  Sikuwa tayari kwa hayo. Niliamua ni njia ambayo mwenyezi Mungu aliamua kunipitisha. Kama mwanaume nilisimama kuhudumia kuhakikisha kwamba mimba inakuwa mpaka anazaliwa binti yangu mrembo, mpenzi wangu wa kwanza, Zuuh Konde. Jambo hilo lilimuumiza mtu ambaye nilikuwa naye kwa mahusiano, Sarah" Harmonize alisimulia.

Harmonize alisema alijaribu sana kuficha mtoto wake katika jitihada za kurejesha mahusiano mazuri na mke wake Sarah.

Staa huyo wa Bongo lifichua kwamba utata mwingi ulizuka kuhusiana na uzazi wa malkia yule hadi akalazimika kufanya vipimo vya DNA baada ya kupata fununu kuwa huenda sio yeye baba mzazi.

"Tulipitia vitu vingi, DNA hivihivi kwa sababu kulikuwa na stori tofauti tofauti. Watu walikuwa wanaleta stori eti sijui mtoto si wangu. Lakini siku zote niliamini baba ni yule mtu ambaye amesimama na mtoto. Siri ya mtoto anayejua ni Mungu. Inawezekana ata mama ya mtoto asijue baba ni nani" Harmonize alisema.