Lilian Ng'ang'a afichua sababu za yeye na Juliani kumuita mtoto wao 'Utheri' (Mwanga)

Mpenzi huyo wa zamani wa Alfred Mutua alisema angependa mwanawe awe mwanga wa dunia.

Muhtasari

•"Ningependa wakati mwanangu akiingia kwenye chumba, kinapata mwangaza mara moja," Lilian alisema.

•Lilian alifichua kuwa watu wamembandika jina Mama Light ilhali Juliani anaitwa Baba Light.

Lilian Ng'ang'a na Juliani
Image: INSTAGRAM// JULIANI

Wiki iliyopita wanandoa Lilian Ng'ang'a na Juliani waliadhimisha miezi miwili tangu kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza pamoja.

Wakati akimsherehekea mwanawe mnamo Septemba 22, Bi Lilian alisema mtoto huyo wake amemletea furaha kubwa kwa kufanya aitwe mama. Aidha alifichua kuwa jina la mwanawe huyo wa mwezi mmoja ni 'Utheri.

"Mnamo 22.07.22 mwendo wa saa 10.11AM, Mvulana mdogo wa ajabu alinipa jina mpya Mama. Leo singesubiri jua ili kuona tabasamu yake ya ajabu huku akitimiza miezi miwili. Utheri mvulana wangu..,” alisema kupitia Instagram. 

Pia alitumia fursa hiyo kumhakikishia mwanawe kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Utheri ni jina la Kikuyu linalomaanisha 'Mwanga.'

Katika mahojiano na Citizen Digital, Lilian alifichua kuwa angependa mwanawe awe mwanga wa dunia.

"Ningependa mwanangu akiingia kwenye chumba, kinapata mwangaza mara moja," alisema.

Alisema kuwa yeye na mumewe Juliani walikuwa makini sana wakati walipomchagulia mwanao jina la 'Utheri' ili atakapokuwa mkubwa limkumbushe kuwa nuru ya ulimwengu.

Aidha alifichua kuwa watu wamembandika jina Mama Light ilhali Juliani anaitwa Baba Light.

Katika mahojiano hayo, mpenzi huyo wa zamani wa Alfred Mutua aliweka wazi kuwa anaifurahia sana ndoa yake na Juliani.

Alisema kuwa anafurahia kuona kwamba hakuna shinikizo analopata katika ndoa hiyo ya takriban mwaka mmoja.

"Ndoa iko poa. Ni rahisi. Naamini ndivyo ndoa inapaswa kuwa. Hata sihisi kama kwamba nimeolewa. Hakuna shinikizo la kujibadilisha kuwa mke. Juliani anaishi maisha yake nami maisha yangu lakini tuko pamoja," alisema.

Lilian na Juliani walitangaza mahusiano yao Septemba mwaka jana, wiki chache tu baada ya Firstlady huyo wa zamani wa Machakos kutangaza kutengana kwake na aliyekuwa gavana, Alfred Mutua.