"Nilikuwa nakufa ndani polepole!" Akothee akumbuka mateso aliyopitia chini ya wazazi wenzake wazungu

"Usiku ningekaa katika vilabu na kurudi nyumbani saa kumi na moja asubuhi ili kuwatayarisha watoto wangu kwa ajili ya shule," alisimulia.

Muhtasari

•Akothee alizungumza kuhusu jinsi alivumilia ndoa na mmoja wa wazazi wenzake kwa sababu tu ya ustawi wa watoto wake.

•Alizungumzia alivyovumilia misukosuko mingi na baba za wanawe na kufichua hakuwahi kuwa na furaha licha ya utajiri wake.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na Mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu safari ya maisha yake na masaibu aliyopitia katika mahusiano na ndoa zake zilizofeli.

Katika chapisho lake la Jumanne asubuhi, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alizungumza kuhusu jinsi alivumilia ndoa na mmoja wa wazazi wenzake kwa sababu tu ya ustawi wa watoto wake.

Alizungumza kuhusu matatizo ambayo alikumbana nayo katika ndoa na mume wake mzungu, jambo ambalo lilimfanya ahisi kana kwamba angetoroka.

“Hakuna haja ya kulea watoto katika ndoa ambayo haipo. Utupu ulio ndani yako utaathiri watoto wako sana. Nikitazama nyuma kwenye picha hizi, naona mwanamke mtupu, mwenye uchungu, aliyepotea. Kitu pekee ambacho kiliweka vipande vyangu pamoja katika uhusiano huu ni ustawi wa watoto wangu.

Nilikuwa nikihesabu mara kwa mara jinsi ya kuepuka fedheha, kelele, na milipuko katika nyumba hii. Ilionekana kana kwamba nilikuwa nikitembea kwenye maganda ya mayai kila mara, nikijaribu kutojikwaa kwa upande mbaya wa mtu yeyote,” Akothee alisema kupitia akaunti yake ya mtandao wa Facebook.

Aliambatanisha taarifa yake na picha za kumbukumbu zake na wanawe wawili nyumbani kwake. Wavulana hao wawili aliowapata na wazunngu wapenzi wake wa zamani walikuwa wadogo sana wakati huo.

Mama huyo wa watoto watano alifichua hayo alipokuwa akiwashauri watu dhidi ya kuiga maisha yake bila kufuata safari ya maisha yake.

Zaidi alizungumzia jinsi alivyovumilia misukosuko mingi na baba za wanawe na kufichua kuwa hakuwahi kuwa na furaha licha ya utajiri wake.

"Niliwapeleka wasichana wangu shule za bweni ili niweze kukabiliana na drama nyuma yao. Nilikuwa na wanaume wawili walinivuruga kichwani kwa jina la malezi ya kushirikiana, mmoja akimlea mtoto wake nje ya uzio, na mwingine mwenye kudhibiti, akipiga kelele tu bila sababu ilibidi niombe ruhusa kwa kila kitu ikiwa ni pamoja na kumpeleka mtoto wake kanisani. 🤔, angenikumbusha kila wakati, "Usisahau mwanangu ni Mkatoliki" 🤔," alisimulia.

Aliongeza, "Familia yangu ilifikiri kwamba nilikuwa nimeshughulikia yote na kwamba, pamoja na pesa zote, nilikuwa nikiishi vizuri sana. Hapana, nyote mmekosea. Nilikuwa nakufa taratibu ndani. Ningekaa usiku katika vilabu na nilirudi nyumbani saa kumi na moja asubuhi ili kuwatayarisha watoto wangu kwa ajili ya shule. Kila niliporudi nyumbani, nilikuwa nikigeuka mita chache tu kutoka kwenye lango langu. Lakini kwa sababu nilifanya maamuzi kulingana na njaa na umaskini, ilinibidi kumeza chura wangu.”

Akothee ana watoto watano, watatu wa kike aliowazaa na mume wake wa kwanza na wana wawili aliowazaa na wanaume wawili tofauti wa kizungu.