Ofweneke adai 1.4M ili kufawidhi harusi ya Akothee kwa kuwa mchumba wake ni mzungu

Akothee alifichua kuwa mchekeshaji huyo amemshauri atafute MC mzungu ikiwa hawezi kulipa pesa alizodai.

Muhtasari

•Akothee amefichua kuwa  Dr Ofweneke anamtoza shilingi milioni 1.4 ili kufawidhi hafla ya harusi yake.

•Aidha alifichua kuwa mchekeshaji huyo amemshauri atafute MC mzungu ikiwa hawezi kulipa pesa alizodai.

DR OFWENEKE, AKOTHEE
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji Akothee ameendelea kudokeza kuhusu mpango wake wa kufunga pingu za maisha na mchumba wake mzungu.

Katika taarifa yake ya hivi punde, amefichua kuwa  Dr Ofweneke anamtoza shilingi milioni 1.4 ili kufawidhi hafla ya harusi yake.

"Wee nilidhani tulikuwa marafiki na @drofweneke, ananichaji 1.4 m kuwa MC rasmi mnamo siku ya harusi yangu, ya kizungu na ya kitamaduni🙄🙄🙄," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 alisema kuwa Ofweneke anadai kiasi kikubwa cha pesa kwa kuwa mchumba wake ni mzungu.

Aidha alifichua kuwa mchekeshaji huyo amemshauri atafute MC mzungu ikiwa hawezi kulipa pesa alizodai.

"Mtu amwambie Dr ofweneke haki sio kwa ubaya ,sikuona yeyote anayenifaa poleni basi 💃💃💃," aliandika.

Chini ya chapisho hilo Ofweneke alimwagiza mama huyo wa watoto watano kulipa nusu ya ada yake kabla ya siku ya harusi.

"Malipo ya awali tafadhali, 50%," alisema.

Akothee aliweka mahusiano yake mapya mapema mwezi huu, miezi michache tu baada ya kutengana na Nelly Oaks.

Tangu kuyafichua mahusiano yake ya sasa mwimbaji huyo amekuwa akijigamba kuyahusu na kudokeza kuhusu harusi hivi karibuni.

Wiki jana aliweka wazi kuwa sasa yuko tayari kuwa mke kwani anahisi kama kwamba maisha yake sasa yamekamilika.

Sikujua kijiji changu kingeweza kuwa Paradiso. Mfalme alikuwa akikosekana. Sasa naweza kusema maisha yangu yamekamilika na niko tayari kutulia, niko tayari kuwa mke mtiifu," Akothee alisema kwenye Instagram.

Takriban miezi mitatu iliyoputa Akothee alithibitisha kutengana kwake na  Bw Oaks baada ya kuchumbiana kwa muda mrefu.