"Maisha yangu yamekamilika, niko tayari kuwa mke mtiifu!" Akothee kuolewa na mpenziwe mzungu

Mwimbaji huyo amesema hatimaye amempata mwenzi wa maisha na yuko tayari kutulia kwenye ndoa.

Muhtasari

•Akothee ameweka wazi kuwa sasa yuko tayari kuwa mke kwani anahisi kama kwamba maisha yake sasa yamekamilika.

•"Jiungeni nasi tukiendelea pamoja hadi kifo kututenganisha," alisema.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Ni wazi kuwa Mwimbaji na Mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee anayafurahia sana mahusiano yake mapya na hivi karibuni huenda tukashuhudia akifunga ndoa na mpenzi wake mzungu.

Siku chache tu baada ya kumtambulisha mpenziwe mpya, mama huyo wa watoto watano sasa amebainisha kuwa baada ya kuhangaika miaka mingi akitafuta mapenzi, hatimaye amempata mwenzi wa maisha na yuko tayari kutulia kwenye ndoa.

Ameweka wazi kuwa sasa yuko tayari kuwa mke kwani anahisi kama kwamba maisha yake sasa yamekamilika.

"Sikujua kijiji changu kingeweza kuwa Paradiso. Mfalme alikuwa akikosekana. Sasa naweza kusema maisha yangu yamekamilika na niko tayari kutulia, niko tayari kuwa mke mtiifu," Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha inayomuonyesha akiwa amekumbatiwa na mpenziwe na kutangaza kwamba walikuwa wakielekea katika mbuga la wanyama la Ruma kwa hafla ambayo hakutoa maelezo zaidi kuhusu.

"Jiungeni nasi tukiendelea pamoja hadi kifo kututenganisha," alisema.

Wikendi mwimbaji huyo aliyezingirwa na utata mwingi aliwatangazia mashabiki wake kuwa tayari amejitosa kwenye mahusiano mengine baada ya kutengana na Nelly Oaks mapema mwaka huu.

"Sipo single tena, unaweza kuwa na uhakika na hilo," alitangaza siku ya Jumamosi.

Aliendelea kumtambulisha rasmi mpenzi wake mzungu kupitia video na kudokeza kuwa tayari amekubali ndoa naye.

Katika maelezo ya video hiyo iliyorekodiwa katika ufukwe wa Bahari la Hindi Akothee alifichua kuwa yeye na mpenziwe walikuwa wamewekelea dau kuwa ikiwa angeweza kumwangusha chini basi atakuwa amekubali ndoa.

"Sawa basi, ni Ndio.. Mtu amwambie mamangu atoke tu kwa kanisa aende nyumbani nilienda kwa date ya chakula cha mchana Mombasa kidogo," aliandika chini ya video hiyo.

Katika video nyingine aliyopakia siku hiyo, mwimbaji huyo alionekana akimbusu mzungu huyo huku akiwa ameficha uso wake. Mikono ya mpenzi huyo wake  ilionekana ikiwa imemkumbatia shingoni.

"Uuuwi mapenzi nouwe, mahaba inizike," alisema.

Haya yanajiri miezi michache tu baada ya mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 kutengana na Nelly Oaks.

Mnamo mwezi Juni Akothee alithibitisha kutengana kwake na  Bw Oaks baada ya kuchumbiana kwa muda mrefu.