(+Video) "Mahaba yanizike!" Akothee azama zaidi kwenye dimbwi la mapenzi na mzungu

Mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa tayari amekubali ndoa na mzungu huyo.

Muhtasari

•Katika video moja, mwanaume mzungu anayeaminika kuwa mpenziwe mpya alisikika akimwambia, "Endelea kumsubiri mama yako."

•Akothee  aliweka dau na mpenziwe kwamba ikiwe angefanikiwa kumwangusha chini basi ni ishara kuwa amekubali ndoa.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee anaonekana kuyafurahia sana mahusiano yake mapya.

Mama huyo wa watoto watano ameendelea kudokeza kuwa tayari ana mpenzi mpya baada ya kutengana na Nelly Oaks. Hata hivyo bado hajafichua sura au jina la mwanaume ambaye ameuteka moyo wake kwa sasa.

Siku ya Jumamosi Akothee alipakia picha na video kadhaa zilizoonyesha akiwa likizoni mjini Mombasa. Wakati huo alikuwa kwenye kundi la watu wasiotambulishwa.

"Chakula cha mchana Mombasa...Mama yangu ananisubiri kanisani," aliandika chini ya video alizopakia kwenye Instastori.

Katika video moja, mwanaume mzungu anayeaminika kuwa mpenziwe mpya alisikika akimwambia, "Endelea kumsubiri mama yako."

Katika video iliyofuata Akothee anaonekana akimbusu mzungu huyo huku akiwa ameficha uso wake. Mikono ya mwanaume huyo asiyetambulishwa mieupe ilionekana ikiwa imemkumbatia shingoni.

"Uuuwi mapenzi nouwe, mahaba inizike," Akothee aliandika chini ya video hiyo.

Katika chapisho lingine, msanii huyo alidokeza kuwa tayari amekubali ndoa na mzungu huyo. Walikuwa wameweka dau kwamba ikiwa mpenziwe angefanikiwa kumwangusha chini basi iwe ishara kuwa amekubali.

"Sawa basi, ni Ndio.. Mtu amwambie mamangu atoke tu kwa kanisa aende nyumbani nilienda kwa date ya chakula cha mchana Mombasa kidogo," Aliandika.

Haya yanajiri miezi michache tu baada ya mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 42 kutengana na Nelly Oaks.

Mnamo mwezi Juni Akothee alithibitisha kutengana kwake na  Bw Oaks baada ya kuchumbiana kwa muda mrefu.

Katika taarifa yake, msanii huyo alibainisha kuwa aliamua kukatisha mahusiano yao na kuzingatia kazi yake na furaha mpya iliyopatikana.

"Nimetoka kwenye mahusiano mengine yenye misukosuko tofauti kwa hivyo hii ya mwisho isiwe ya kushtua au ya kushangaza. Ni uamuzi wa kibinafsi tu, ninahitaji wakati wa kuzingatia furaha yangu mpya iliyopatikana na uharibifu mdogo, ninahitaji kujishughulisha mwenyewe na kazi yangu," alisema.

Aidha aliweka wazi kuwa hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi kuhusu kilichovunja mahusiano yake na meneja huyo wake wa zamani.