Ruth K alalamika kuhusu jinsi mwanawe anavyofanana sana na Mulamwah

Mpenzi huyo wa Mulamwah alibainisha kwamba mwanawe Oyando Jr hafanani naye.

Muhtasari

•Ruth alidokeza kwamba hata vidole vya miguu na mikono vya mtoto huyo wake wa wiki chache vinafanana na vya Mulamwah.

•Pia alilalamika kuhusu jinsi mtoto wake mchanga amempunguzia muda wake wa kulala.

Mulamwah na mpenzi wake Ruth K
Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mtayarishaji wa maudhui Ruth K alilalamika kwa utani kuhusu ufanano mkubwa wa mwanawe na mzazi mwenzake David Oyando almaarufu Kendrick Mulamwah.

Akizungumza kwenye video aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa mtoto mmoja alibainisha kuwa mwanawe Oyando Jr hafanani naye.

Alidokeza kwamba hata vidole vya miguu na mikono vya mtoto huyo wake wa wiki chache vinafanana na vya Mulamwah.

“Ona mnafanana hadi vidole. Si hanifanani. Wee angalia tu mikono na miguu,” Ruth K alisikika akimwambia mpenzi wake Mulamwah.

Wakati akimjibu mpenzi wake, Mulamwah alimwambia ,” Ongeza bidii”, ushauri ambao Ruth K aliuliza jinsi ungewezekana.

Katika video hiyo, mrembo huyo mtayarishaji wa maudhui alionekana akiwa amemshika mwanawe akiwa ameketi kwenye balcony ya nyumba yao mpya jijini Nairobi.

Alisikika akishiriki mazungumzo na mzazi mwenzake ambapo pia alilalamika kuhusu jinsi mtoto wake mchanga amempunguzia muda wake wa kulala.

“Sasa hivi nikuota tu jua na Kalamwah tupate vitamin D. Aki lakini nimekesha.. unajua wewe unalala tu. Wewe ulimaliza shift mapema. Unafaa unaongeza muda,” Ruth alimwambia Mulamwah.

Haya yanajiri siku chache baada ya wapenzi hao kuhama kutoka nyumba aina ya bedsitter ambayo Mulamwah amekuwa akiishi kwa muda mrefu.

Katika taarifa yake, mchekeshaji huyo alidokeza kwamba walilazimika kuhamia katika nyumba ya vyumba vitatu vya kulala ili kupata mazingira bora ya kulea mtoto wao.

Mulamwah na mpenzi wake Ruth K walitangaza kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza pamoja takriban wiki mbili zilizopita.

Wakati akitangaza habari hiyo njema, Mulamwah alieleza dhamira yake kubwa katika kujenga kumbukumbu na mwanawe.

“MUNGU NI MKUU , hatimaye kijana wetu yuko hapa , mrithi yuko hapa , MFALME yuko hapa - @oyando_jnr aka kalamwah, karibu duniani mwanangu, ni hisia nzuri zaidi ulimwenguni hatimaye kukuona na kukushikilia. siwezi kusubiri sisi kukua na kufanya kumbukumbu pamoja, "alisema.

Pia alimtambua mzazi mwenzake Ruth K, na kumshukuru kwa kumpa mtoto wake wa pili na kuwa naye kila wakati.

"Asante sana @atruthk kwa zawadi hii nzuri na ya kushangaza, asante kwa kuwa karibu nami kila wakati," alisema.

Aliongeza, “Ninahisi mzima tena, nahisi kurejeshwa, nina furaha , familia sasa zina furaha dunia nzima ina furaha , ♥️♥️ . Nakutakia maisha marefu na yenye afya tele kijana wangu na kila la kheri ulimwenguni. baraka tele. Karibu KALAMWAH !! maisha marefu oyando.”