"Sitaki nisikie analia mitandaoni" Stivo amshauri Vishy baada ya kunyakuliwa na msanii mwingine

Stivo amemuonya Madini dhidi ya kuumiza moyo wa mpenzi huyo wake wa zamani.

Muhtasari

•Vishy ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 20 anadaiwa kuwa kwenye mahusiano na mwanamuziki Madini Classic.

•Stivo amemtakia kheri njema mpenzi huyo wake wa zamani katika mahusiano yake mapya na kumshauri atulie.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy anaripotiwa kuwa amezama kwenye dimbwi la mahaba.

Vishy ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 20 anadaiwa kuwa kwenye mahusiano na mwanamuziki Madini Classic.

Wawili hao tayari wamethibitisha kuwa wanachumbiana  huku Vishy akiweka wazi jinsi anavyofurahia mahusiano yao.

"Ninafurahia kuwa naye na ninafurahia mambo mapya ambayo ninapata. Kitu ambacho sijawahi kupata kutoka kwa mahusiano ya awali angalau. Kwa hiyo hata kwangu naweza kusema kwa ujasiri kwamba ninapendwa na niko katika upendo," Vishy alisema katika video iliyopakiwa YouTube.

Vishy na Madini waliweka mahusiano yao hadharani takriban wiki moja iliyopita.

Kwa mara ya kwanza Stivo Simple Boy amevunja kimya chake kuhusiana na hatua hiyo ya mpenzi wake wa zamani.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Stivo alimtakia kheri njema kipusa huyo na kumshauri atulie kwenye mahusiano yake mapya.

"Kama anapenda yule mpenzi ambaye anapenda kwa dhati, ashikilie. Bora tu si kudanganyana," Stivo alisema.

Rapa huyo kutoka Kibra pia alimuonya Madini Classic dhidi ya kuumiza moyo wa mpenzi huyo wake wa zamani.

"Sitaki nisikie Pritty analia kwa mtandao ati heri ningekuwa na Simple Boy. Sitaki," Alisema.

Stivo na Vishy walitengana mwezi Machi mwaka huu baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu.

Mwanamuziki huyo ameweka wazi kuwa Vishy ndiye aliyechukua hatua ya kukatiza mahusiano yao na kumuacha.

"Yeye ndio aliamua kuniacha. Nilishtukia mtu ashamove on bila kusema sababu ni gani," Alisema Stivo.

Wakati huohuo Stivo ametangaza mipango ya harusi yake na mpenzi wake wa sasa ambaye hajamtambulisha.

Rapa huyo ametangaza kwamba hatimaye amepata mpenzi waa maisha yake ambaye ametimiza yote aliyotarajia.

"Nimepata ambaye nilikuwa natarajia kwa maisha yangu. Mlango moja ikifunguka, ingine inafungulia. Nashukuru Mungu kwa kunipa mtu ambaye nilikuwa natarajia kwa maisha yangu," Alisema.

Pia alifichua kuwa alianza kuchumbiana na mchumba wake bado akiwa kwenye mahusiano na Vishy.