"Siwezi kustahimili maumivu haya!" Akothee alaani kisa cha mwanadada Mkenya kunyonyesha mbwa Saudi Arabia

"Sisi kama nchi tunapaswa kushughulikia hili. Maisha ya wanawake ni muhimu." alisema.

Muhtasari

•Akothee amekosoa kitendo hicho na kusema Kenya inafaa kuyashughulikia na kuchukua hatua kali kuhusu masuala kama hayo ambayo yamekithiri siku za hivi majuzi.

•Aliweka wazi kuwa matukio ya kusikitisha kama hayo yanamuumiza sana moyoni kwa kuwa pia yeye ni mama.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Wakenya wameendelea kutoa maoni baada ya video inayodaiwa kuwa ya mwanamke Mkenya akiteseka katika mojawapo ya nchi za Mashariki ya Kati kusambaa mitandaoni.

Katika video hiyo ambayo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, mwanadada anayeonekana akinyonyesha mbwa alifichua kwamba mwajiri wake alimwagiza afanye vile baada ya kugundua kuwa alikuwa mama mpya.

Radio Jambo hata hivyo haiwezi kuthibitisha uhalisi wa video hiyo.

Mwimbaji na mjasiriamali Akothee ndiye mtu mashuhuri wa hivi punde kuvunja ukimya wake kuhusu suala hilo. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watano amekosoa kitendo hicho na kusema Kenya inafaa kuyashughulikia na kuchukua hatua kali kuhusu masuala kama hayo ambayo yamekithiri siku za hivi majuzi.

"Ni akina nani hawa wanaopeleka wasichana wetu kwenye nchi zisizo na ubinadamu,nini hiyo nimetazama sasa? Mama ananyonyesha mbwa? Na alimwacha mtoto wake mwenyewe nyumbani!" alilalamika.

Aliongeza, "Sisi kama nchi tunapaswa kushughulikia hili. Maisha ya wanawake ni muhimu."

Mwimbaji huyo aliendelea kutaka mashirika yanayohusika na kupeleka wasichana nje ya nchi kuwa wazi na maelezo ya wale ambao  yametuma tayari.

"Tunataka kuwasiliana nao kwa video na kuzungumza nao kutoka Kenya, tunataka kuongea na mabosi wao na kujua kama wako sawa. Tunahitaji mawasiliano ya kila mwanamke Mkenya katika Mashariki ya Kati," alisema.

Aliweka wazi kuwa matukio ya kusikitisha kama hayo yanamuumiza sana moyoni kwa kuwa pia yeye ni mama.

"Siwezi kuvumilia maumivu haya kama mama," alisema.

Hii yalijiri kipindi kifupi baada ya Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli kuomba serikali kupiga marufuku mashirika yote yanayopanga nafasi za kazi katika mataifa ya kigeni.

Matamshi yake yalikuja  baada ya kupokea video hiyo ya mwanamke Mkenya akinyonyesha mbwa nchini Saudi Arabia.

Alisema kuna haja ya kuwalinda wafanyikazi kutoka Kenya na hilo linaweza kufikiwa kwa kupiga marufuku mashirika yanayokuza kazi za nje ya nchi, haswa nchini Saudi Arabia.

"Ninataka kutoa wito kwa serikali yetu kufuata jinsi serikali ya kwanza ya Rais Mwai Kibaki chini ya Waziri wa Leba Phyllis Kandie alivyofanya. Ilipiga marufuku mashirika yote ya ajira nchini Kenya," alisema.

Atwoli alizungumza na wanahabari Jumapili nyumbani kwake Kajiado. liongeza kuwa, serikali inapaswa pia kufanya mazungumzo na serikali ya Saudi Arabia kuhusu masharti ya utumishi iwe nchini Qatar au popote pale Mashariki ya Kati.

"Hii ni ili watu wetu wanaoishi katika nchi hii waweze kufanya kazi zenye heshima," alisema.

Kuhusu mwanamke ambaye alirekodiwa akinyonyesha mbwa, Atwoli alisema aliondoka Kenya miezi miwili baada ya kujifungua.

"Walipogundua kuwa anaweza kunyonyesha, mwajiri badala ya kumpa kazi ifaayo, alimpa msichana huyu kazi ya kunyonyesha watoto wa mbwa wake. Huu ni utumwa usio wa moja kwa moja."

Atwoli aliendelea kusema kwamba jinsi wafanyikazi hutendewa katika mataifa ya Mashariki ya Kati huwanyima utu na heshima ambayo wanapaswa kupewa kama wanadamu na Wakenya.