Miguna amshambulia Atwoli kwa ajili ya dhuluma wanazopokea Wakenya nje za nchi

Miguna alimshutumu Atwoli kwa kushindwa kutimiza wajibu wake uliomtaka kutetea haki za wafanyikazi ndani na nje ya nchi.

Muhtasari
  • Atwoli Jumapili alimtaka Rais William Ruto kupiga marufuku mashirika yote ya uajiri akisema yamefeli Wakenya
Image: TWITTER// MIGUNA MIGUNA

Wakili Miguna Miguna sasa anasema kwamba Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli anafaa kutumikia kifungo kwa kuzembea majukumu yake.

Katika taarifa yake siku ya Jumapili, Miguna alimshutumu Atwoli kwa kushindwa kutimiza wajibu wake uliomtaka kutetea haki za wafanyikazi ndani na nje ya nchi.

Maoni yake yanakuja baada ya Atwoli kufanya mkutano na wanahabari akitaka mashirika yote ya kuajiri yanayobadilisha nafasi za ajira kwa wafanyikazi wa Kenya walio nje ya nchi kufungwa.

Hii ni baada ya kupokea rekodi ya video ya mwanamke Mkenya akinyonyesha mbwa.

"Francis Atwoli amekuwa wapi kwa miaka 10 iliyopita ambapo wanawake wa Kenya wamesafirishwa, kugeuzwa watumwa, kushushwa hadhi, kuteswa, kulemazwa na kuuawa katika nchi za Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Yemen, Lebanon na nchi nyingine za Mashariki ya Kati?" Aliuliza.

"Atwoli anastahili miaka 500 huko Kamiti."

Atwoli Jumapili alimtaka Rais William Ruto kupiga marufuku mashirika yote ya uajiri akisema yamefeli Wakenya.

"Ninataka kutoa wito kwa serikali yetu kufuata jinsi serikali ya kwanza ya Rais Mwai Kibaki chini ya Phyllis Kandie alivyofanya Waziri wa Leba. Ilipiga marufuku mashirika yote ya ajira nchini Kenya," alisema.