Vera Sidika afunguka kuhusu kutoa mimba ya Otile Brown, kwa nini hapendi muziki wake

"Unawezaje kutoa mimba ambayo haikuwahi kuwepo?" alihoji.

Muhtasari

•Mwanasoshalaiti huyo alibainisha kuwa hakuwahi kuwa mjamzito wakati wa mahusiano yake na Otile Brown.

•Mama huyo wa binti mmoja alisema kutosikiliza nyimbo za Otile Brown hakumaanishi kwamba anamchukia.

Vera Sidika na Otile Brown wakati wa mahusiano yao
Image: HISANI

Siku ya Jumamosi, mwanasholaiti maarufu Vera Sidika aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram ambapo alijibu maswali mbalimbali kuhusu maisha yake kuanzia ndoa, uzazi, kazi n.k.

Vera hakulazimika tu kuzungumzia ndoa yake ya sasa na mwimbaji Fredrick Mutinda almaarufu Brown Mauzo, bali pia kuhusu mahusiano ya zamani na Otile Brown. Wawili hao walichumbiana miezi kadhaa kabla ya kutengana 2018.

Shabiki mmoja alimtaka ajibu madai kwamba alitoa ujauzito wa mwanamuziki huyo mzaliwa wa pwani wakati wa mahusiano yao.

"Ni kweli ulitoa mimba ya mtoto wa Otile Brown?" shabiki aliuliza.

Katika jibu lake, mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 33 alibainisha kuwa hakuwahi kuwa mjamzito wakati wa mahusiano yake na Otile Brown. Pia aliweka wazi kuwa kamwe hawezi kutoa mimba.

"Unawezaje kutoa mimba ambayo haikuwahi kuwepo? Kusema kweli, siwezi kufanya biashara hii. Ninapenda watoto sana. Ninaweza kupat 10 kama ningeweza," alisema.

Katika wimbo wake 'Niacheni' ambao aliachia miaka kadhaa iliyopita, mwimbaji Otile Brown alidokeza kuwa alitoka kwenye mahusiano fulani baada ya mwanamke aliyekuwa akichumbiana naye kutoa mimba.

Mashabiki wake waliamini alimzungumzia Vera Sidika katika wimbo huo wa hisia alioutoa baada ya kutengana kwao.

“Usijifanye eti hujui, Tatizo mimba yangu ulioitoa, Mimi niacheni msione nipo kimya mwenzangu nina mengi. Wacha nilie na moyo wangu maneno maneno mimi sipendi. Nitafanya vizuri zaidi", Otile aliimba.

Akijibu madai hayo mwaka wa 2021, Vera alikana kuwahi kuwa mjamzito hapo awali na kuweka wazi upendo wake kwa watoto.

Wakati wa kipindi cha maswali na majibu, alipoulizwa kwa nini anamchukia mpenzi huyo wake wa zamani , mama huyo wa binti mmoja alisema kutosikiliza nyimbo zake hakumaanishi kwamba anamchukia.

“Sina chuki, napendelea zaidi kusikiliza muziki wa mume wangu na hiyo haimaanishi kuwa nachukia,” alijibu baada ya kuulizwa kwa nini huwa hasikilizi kabisa nyimbo za mpenzi wake wa zamani, Otile Brown.

Kwenye mahojiano na Massawe Japanni mwaka jana, Vera alifichua kwamba alikuwa amekataa tamaa ya kujitosa kwenye mahusiano na mtu maarufu.

Alisema hakutazamia kuchumbiana na msanii mwingine yeyote baada ya mahusiano yake na Otile Brown kugonga mwamba mwakani 2018.

"Nilihisi sitaki kuwa na mahusiano na mtu ambaye ni maarufu!" alisema.