Mwanamuziki Otile Brown afichua kwa nini anaipenda Ethiopia

Brown alizikosoa nchi ambazo zimeacha tamaduni zao na kuchukua za wengine.

Muhtasari

•Otile Brown alisafiri kuelekea nchi hiyo ya Afrika Kaskazini Mashariki mwa Afrika wiki iliyopita ila hakufichua nia ya  ziara yake.

Msanii wa kizazi kipya Otile Brown katika mahojiano ndani ya rdio Jambo.
Msanii wa kizazi kipya Otile Brown katika mahojiano ndani ya rdio Jambo.
Image: Radio Jambo (Facebook)

Mwanamuziki mahiri wa Kenya Jacob Obunga almaarufu Otile Brown amekuwa nchini Ethiopia kwa siku kadhaa ambazo zimepita.

Otile Brown alisafiri kuelekea nchi hiyo ya Afrika Kaskazini Mashariki mwa Afrika wiki iliyopita ila hakufichua nia ya  ziara yake.

Kulingana na machapisho yake ya hivi majuzi kwenye mtandao wa  Instagram, mwanamuziki huyo mzaliwa wa eneo la Pwani, Kenya anaonekana kufurahia ziara yake ya Ethiopia. Siku ya Ijumaa alichapisha video kadhaa zikimuonyesha akijiburudisha na kusherehekea katika klabu moja katika nchi  hiyo ya kigeni.

"Arrow Bwoy/Harmonize anapiga kali nchini Ethiopia, wanapaswa kukata cheki haraka iwezekanavyo,"  Aliandika chini ya video yake akifurahia wimbo wa Harmonize, Diamond na Burna Boy 'Kainama katika kilabu.

Video zingine alizochapisha zilimuonyesha akifurahia nyimbo za Ethiopia zilizochezwa katika klabu hiyo. Alionekana akiwa pamoja na wanawake kadhaa wasiotambulishwa.

Katika mojawapo ya posti zake alifichua kuwa anaipenda Ethiopia kwa sababu ya jinsi wamedumisha utamaduni wao. Alichukua fursa hiyo kuzikosoa nchi ambazo zimeacha tamaduni zao na kuchukua za wengine.

"Nchi isiyo na tamaduni imepotea.. Najihusisha sana na Ethiopia kwa sababu hawachezi linapokuja suala la utamaduni wao,"  alisema.

Ni wazi kwamba mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 ana upendo mkubwa kwa Ethiopia. Takriban mwaka mmoja uliopita alikuwa akichumbiana na mrembo wa Ethiopia, Nabayet aka Nabbi ambaye alitengana naye baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa takribana miaka mitatu.

Mapema wiki hii kulikuwa na tetesi nyingi kwenye mitandao ya kijamii kwamba  alizuru nchi hiyo ili kumuona Nabbi. Wapelelezi wa mitandaoni walifanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa wawili hao walikutana.

Siku ya Jumanne, Brown alichapisha picha yake akiwa amesimama nje ya nyumba moja katika mji mkuu wa Ethiopia. Pichani alikuwa amevalia shati nyeupe, t-shati nyeusi, suruali nyeusi na kiatu cheupe huku akiwa amebeba mkoba.

"Soma maisha...," aliandika chini ya picha hiyo.

Nabayet, ambaye ni mzaliwa wa Ethiopia, pia alichapisha picha  ambayo ilimuonyesha akiwa katika hoteli moja jijini Addis Ababa.

Kwenye picha, mkono wa mwanaume uliokuwa na pete kwenye kidole cha pete ulionekana. Pia, mwanamume huyo alikuwa amevalia shati jeupe na wanamitandao wamefanikiwa kumtambua kuwa sio mwingine bali ni Otile Brown.