"Inauma ila nimefanya kwa ajili yako" Rayvanny akiri kwa mpenziwe baada ya kuchorwa jina lake

"Umekuwa mwanamke wa tofauti kwangu, nakuheshimu," Rayvanny alimwambia Fahyma.

Muhtasari

•Rayvanny alidhihirisha mapenzi yake kwa mwanamitindo huyo kwa kuchorwa jina lake kwenye kifundo cha mkono wake.

•Alibainisha kwamba iwapo watu wangeelewa mapenzi yake kwa mwanamitindo huyo basi wangeelewa hatua hiyo yake.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Ni wazi kuwa wapenzi na wazazi wenza mashuhuri, Rayvanny na Fahyma wamezama kabisa kwenye dimbwi la mahaba mazito.

Siku ya Alhamisi, Rayvanny alidhihirisha mapenzi yake kwa mwanamitindo huyo kwa kuchorwa jina lake kwenye kifundo cha mkono wake.

"Fahyma...❤," ilisomeka tattoo mpya ya mwimbaji huyo.

Bosi huyo wa Next Level Music alionyesha video yake akichorwa katika duka moja la tattoo jijini Arusha, Tanzania na akaweka wazi kwamba alichukua hatua hiyo kutokana na mapenzi yake makubwa kwa mzazi huyo mwenzake.

Alisema, licha ya kuwa ni chungu, alilazimika kufanya hivyo kutokana na athari kubwa ya Fahyma katika maisha yake.

"Inauma sana ila nimefanya hivi kwa ajili yako Fahvanny," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Aliongeza, "Umekuwa mwanamke wa tofauti kwangu, nakuheshimu."

Alibainisha kwamba iwapo watu wangeelewa mapenzi yake kwa mwanamitindo huyo basi wangeelewa hatua hiyo yake.

"Hata ungekuwa wewe ungechora tu," alisema.

Huku akimshukuru mwimbaji huyo wa Bongo, Fahyma alikiri upendo wake mkubwa kwake.

"Nakupenda, nashukuru sana maisha yangu," alisema.

Haya yanajiri takriban wiki mbili baada ya wawili hao kuthibitisha kurudiana kwao, takriban miaka mitatu baada ya kutengana.

Wawili hao walithibisha kufufuka kwa mahusiano yao yaliyosambaratika takriban miaka mitatu iliyopita, siku chache zilizopita baada ya Rayvanny kumshirikisha mpenziwe huyo katika video ya wimbo wake mpya 'Forever.'

“Mtoto mbichi teketeke aki Mama umelainika. Umeumbika, acha nikumwagie sifa. Waruke sakara na mateke uzuri wako hawatofika, mama umejazisha, mikate ya kumiminisha,” Rayvanny alimsfia Fahyma kwenye wimbo huo.

Siku chache baada ya kuachia wimbo huo, bosi huyo wa Next Level Music alithibitisha  wanaishi pamoja baada ya kurudiana.

Siku ya Jumapili, staa huyo wa Bongo alikiri jinsi anavyom'miss mpenzi huyo wake baada ya kusafiri kuenda mbali naye.

Rayvanny alichapisha  video inayomuonyesha akimsindikiza mama huyo wa mtoto mmoja hadi uwanja wa ndege na kumuaga.

"Nimekumiss, si urudi basi @fayvanny," aliandika chini ya video hiyo,

Hata hivyo, hakufichua maelezo ya safari ya mpenzi huyo wake  hivyo alikoelekea na alichoenda kufanya bado ni kitendawili.