Hatutaki mapendeleo, lazima nishinde tuzo - Babalevo

Muhtasari

• Msanii na mtangazaji tokea taifa la Tanzania, Babalevo amesema kwamba lazima awe mshindi katika tuzo zilizozinduliwa na BASATA majuzi, tuzo ambazo zitawashuhudia wasanii wakituzwa katika vitengo tofauti.

• Aidha, akichapisha ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram, Babalevo ameonya kwamba mara hii hawataki upendeleo katika utoaji wa tuzo hizo na kwamba kila msanii awe na mazingira sawa ya kuwania bila kushurutishwa kwa namna yoyote ile.

• ‘Dokta’ kama anavyotambulika kwa sasa pale Bongo, msanii huyo anazidi kufanya vizuri huku akitia kibindoni hela nyingi kupitia mikataba ya ubalozi kwa kampuni mbalimbali.

Msanii na mtangazaji kutoka Tanzania, Babalevo amesema kwamba lazima awe mshindi katika tuzo zilizozinduliwa na BASATA majuzi, tuzo ambazo zitawashuhudia wasanii wakituzwa katika vitengo tofauti.

Babalevo ambaye amekuwa na rekodi nzuri kimuziki tangu awe na ukaribu na bosi wake, Diamond Platinumz , ameahidi kufanya kila awezalo kutoa muziki mzuri ili kuhakikisha kwamba anahifadhi nafasi yake kwenye tuzo hizo.

Aidha, akichapisha ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram, Babalevo ameonya kwamba mara hii hawataki upendeleo katika utoaji wa tuzo hizo na kwamba kila msanii awe na mazingira sawa ya kuwania bila kushurutishwa kwa namna yoyote ile.

Hata hivyo swali kubwa ni kuwa, atawezaje kumpiku bosi wake ambaye amekuwa akimshabikia kwa muda mrefu sasa, na pia ni kipi atafanya tofauti ili kutoa upinzani miongoni mwa mastaa wengine ambao watashirki katika tuzo hizo.

‘Dokta’ kama anavyotambulika kwa sasa pale Bongo, msanii huyo anazidi kufanya vizuri huku akitia kibindoni hela nyingi kupitia mikataba ya ubalozi kwa kampuni mbalimbali. La mno kwa sasa ni kusubiria mbivu na mbichi litakayoshuhudiwa miongoni mwa mastaa hao wa Tanzania kwenye tuzo hizo.