"Haijakuwa rahisi, Haitakuwa rahisi," Mkewe Bien azungumzia ndoa yao ya miaka miwili

Muhtasari

•Bien na Kuruka walichumbiana kwa kipindi cha takriban  miaka sita kabla ya kufunga pingu za maisha mnamo Machi 2020.

•Chiki amekiri kuwa ndoa yao haijakuwa rahisi ila akaashiria kuwa angependa watengeneze kumbukumbu zaidi pamoja.

Image: INSTAGRAM// CHIKI KURUKA

Siku ya Jumapili mwanamuziki wa bendi ya Sauti Sol Bien na mke wake Chiki Kuruka waliadhimisha miaka miwili  ya ndoa yao.

Bien na Kuruka walichumbiana kwa kipindi cha takriban  miaka sita kabla ya kufunga pingu za maisha mnamo Machi 2020.

Wanandoa hao walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kusherehekeana kwa hatua ambazo wamepiga pamoja.

Bi Kuruka alimhakikishia mumewe kuhusu mapenzi yake kwake huku akitaja sababu zilizofanya amchague msanii huyo kama mshirika wake wa maisha.

Kuruka alikiri kuwa ndoa yao haijakuwa rahisi ila akaashiria kuwa angependa watengeneze kumbukumbu zaidi pamoja.

"Miaka 2 ya ndoa.... Miaka 8 ya mapenzi. Wewe ni mtu wangu, Kwa nini? Kwa sababu mantiki yangu inalingana na hisia zangu na wewe. Kihisia, hakuna mtu anayenifanya nijisikie mrembo, mwenye akili, mwenye nguvu na kupita ubinadamu kama wewe. Na kimantiki, najua mimi ni tolea langu bora zaidi nikiwa na wewe. Ninajua hitaji lako la kujisikia huru, inamaanisha kuwa ninabaki huru. Uwezo wako wa kunipuuzilia, inamaanisha kuwa sijawekwa katika njia zangu. Kupigana kwako mwenyewe, kunanikumbusha kujipigania mwenyewe. Haijawa rahisi kila wakati, na nina hakika haitakuwa rahisi kila wakati. Lakini pia nina hakika, kwamba wewe na wewe peke yako, ni mtu wangu (uko sawa kabia ) Kwa matukio mengi zaidi 🥂🥂. Furaha ya maadhimisho ya ndoa!," Kuruka alisema.

Bien kwa  upande wake alisema anajihisi mwenye bahati kubwa kuwa na Bi Kuruka maishani huku akimtaja mkewe kama dira yake ya maisha.

Heri za maadhimisho ya ndoa kwa mpenzi wa maisha yangu. Tumeoana kwa miezi 24.🤣🤣🤣Ningeweza kuandika kitabu kuhusu jinsi nina bahati kuwa na wewe maishani mwangu. Kwa kweli unatoa yaliyo bora ndani yangu. Kwa kumbukumbu nyingi zaidi mpenzi wangu. Asante kwa  kuwa dira yangu. Nakupenda na nakuthamini," Bien aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Wawili hao walifunga pingu za maisha  katika hafla ya faragha iliyofanyika tarehe 6 Machi 2020. Chiki pia ndiye meneja wa Bien.