Ibraah aingia jukwaani kwa jeneza katika Afro East Carnival

Muhtasari

• Msanii Ibrah amechukua mtindo wa Khaligraph Jones wa kuingia jukwaani ndani ya jeneza.

• Alitokea ndani ya jenezxa na kujitupa jukwaani wakati wa tamasha ya Harmonize ya Afro East Carnival.

Ibraah
Image: Instagram

Mwanamuziki wa Konde Gang Ibraah aliwashangaza wengi baada ya kuingia jukwaaani akiwa ndani ya jeneza katika tamasha la Afro East Carnival lake msanii Harmonize lililofanyika Machi 5, Tabata nchini Tanzania.

Mashabiki wake wengi waliokuwa wakimsubiria kuingia jukwaani baada ya jina lake kuitwa walistaajabu walipoona jeneza jeupe likisukumwa jukwaani na baadae lilipofunguliwa msanii Ibraah akatokea ndani na kuwaacha wengi vinywa wazi huku  tukio hilo likizua maoni kinzani kwa umati.

Baadhi waliusifia mtindo wake huo wa kuingia jukwaani ambao waliutaja kuwa wa kipekee na wenye ubunifu mkubwa huku wengine wakimsuta kwa kutumia suala la jeneza na kifo kama mzaha katika tamasha.

Walisema haifai jeneza kutumiwa katika mambo ya mizaha kama hiyo kwani kifo si kitu cha kuchezea shere kwa sababu matukio kama hayo huonesha huzuni na simanzi ya kuondokewa na mpendwa.

Hii si mara ya kwanza kwa wasanii kujitupa jukwaani wakiwa ndani ya jeneza kwani miaka minne iliyopita msanii wa rap kutoka nchini Kenya, Khaligraph Jones aliingia jukwaani akiwa ndani ya jeneza jeupe katika tamasha ya Jameson iliyoandaliwa kwenye ukumbi wa Uhuru Gardens jijini Nairobi.

Jones pia alikuwa tayari ashaachia kibao kimoja kwa jina Gaza ambapo pia alionekana na jeneza hilo jeupe ambapo alijitetea kwa wafuasi wake waliotaka kujua kiini cha yeye kutumia jeneza kimzaha na kusema kwamba alikuwa anataka kufikisha ujumbe kwa vijana kwamba ujambazi unagharimu maisha ya vijana wengi katika mitaa ya Nairobi.

Je, unahisi wasanii kutumia majeneza katika tamasha na video zao ni halali ama ni mikosi wanajitafutia?