Sijashiriki tendo la ndoa tangu 2013- Robert Burale afunguka

Muhtasari

•Burale alisema amekuwa akijiepusha na ngono tangu alipotengana na mkewe takriban miaka tisa iliyopita.

•Alisema alipata masomo mengi kutoka kwa ndoa yake ya kwanza ambayo anatarajia kutumia katika ndoa yake nyingine.

Image: INSTAGRAM//ROBERT BURALE

Mshauri na mhubiri mashuhuri nchini Robert Burale amekiri kwamba hajawahi kushiriki tendo la ndoa na yeyote tangu ndoa yake iliposambaratika.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Burale alisema amekuwa akijiepusha na ngono tangu alipotengana na mkewe takriban miaka tisa iliyopita.

"Sijashiriki mapenzi tangu ndoa yangu igonge ukuta. Sijakuwa katika ndoa tangu 2013. Ni Mungu," Burale alisema.

Mkufunzi huyo wa masuala  ya kimaisha alisema kwamba ngono ni kitendo takatifu ambacho kimehifadhiwa tu kwa wanandoa.

Burale alikiri kwamba anatamani sana kujitosa tena kwenye ndoa. Hata hivyo hakufichua wakati ambapo anatarajia kumvisha mwanamke mwingine pete.

"Sina neema ya kuwa single. Natamani ndoa. Itafanyika. Wale wanaosema utaoa lini, nikioa watasema utapata mtoto mwingine lini. Huwezi kutosheleza kila mtu," Alisema.

Burale alimsifia sana aliyekuwa mkewe huku akimtaja kama mtu mzuri. Alisema alipata masomo mengi kutoka kwa ndoa yake ya kwanza ambayo anatarajia kutumia katika ndoa yake nyingine.