Harmonize azungumza kuhusu mipango yake ya kisiasa

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alidokeza kuwa huenda akajitosa kwenye ulingo wa siasa  katika siku za usoni.

•Takriban miaka mitatu iliyopita, rais Magufuli alimhimiza Harmonize kujaribu bahati yake katika siasa.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize ameweka wazi kwamba hayupo tayari kujitosa kwenye siasa licha ya kuwa na ushawishi mkubwa.

Akihutubia wanahabari siku ya Jumapili, Harmonize hata hivyo alidokeza kuwa huenda akageuka kuwa mwanasiasa katika siku za usoni.

"Siko tayari kujiingiza kwenye siasa bado lakini Inshallah panapo Majaliwa katika siku za mbeleni huko," Harmonize alisema.

Mwanamuziki huyo alimsifia rais wa zamani wa Tanzania  John Pombe Magufuli huku akifichua kwamba hayati alimpa msukumo mkubwa.

Takriban miaka mitatu iliyopita, rais Magufuli alimhimiza Harmonize kujaribu bahati yake katika siasa.

Magufuli aliliongeza uzito ombi la wakazi wa Mtwara kwa mwanamuziki huyo kuwawakilisha bungeni.

“Nampongeza sana Harmonize. Sijui anatoka Jimbo gani, anatoka jimbo gani huyu? Tandahimba? Mbunge wa kule ni nani? Ningetamani kweli Harmonize aende akagombee kule awe mbunge wa Tandahimba," Magufuli alisema.

Harmonize ameapa kuendelea kumsherehekea hayati Magufuli huku akiahidi kuthamini na kufuatilia maono yake.