"Nitaendelea kuikumbuka familia yake," Harmonize amsherehekea hayati John Magufuli

Muhtasari

• Harmonize alisema rais huyo wa tano wa Tanzania ambaye alifariki mwaka mmoja uliopita alimpa msukumo mkubwa wa kimaisha wakati alipokuwa hai.

•Harmonize alifichua kuwa uhusiano wake na mjane wa Magufuli, BiJanet Magufuli ni kama wa mama na mwanawe.

Harmonize na hayati John Magufuli
Harmonize na hayati John Magufuli
Image: HISANI

Mwanamuziki wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameapa kuendelea kusherehekea maisha ya aliyekuwa rais wa Tanzania, hayati John Pombe Magufuli.

Akihutubia waandishi wa habari siku ya Jumapili, Harmonize alisema rais huyo wa tano wa Tanzania ambaye alifariki mwaka mmoja uliopita alimpa msukumo mkubwa wa kimaisha wakati alipokuwa hai.

"Ule mguso alionigusa unafanya mpaka leo nitambue na niheshimu uwepo wake. Haijalishi kwamba yupo mzima au hatupo naye tena. Nitaendelea kuenzi yale mazuri yake na pia nitaendelea kuikumbuka familia yake. Kama alikuwa anaweza  kutenga muda wake na kunipigia simu kunijulia hali akiwa rais wa nchi ya zaidi ya watu milioni 60 akaona anipigie mimi, inaamisha kwamba kuna kitu kilikuwa ndani yake," Harmonize alisema.

Harmonize alisema kando na msukumo, hayati Magufuli pia alimfanya aaminike zaidi katika jamii ya Watanzania.

Aliahidi kuendelea kuwa karibu na familia ya Magufuli na kufuatilia maono yake kadri awezavyo. Alifichua kuwa uhusiano wake na mjane wa Magufuli, Janet ni kama wa mama na mwanawe.