Diamond ajibu madai ya kumshusha na kumroga Harmonize

Muhtasari

•Diamond alikana kuwahi kujaribu kumshusha Harmonize ama kumwagiza atoe kitita kikubwa cha pesa alipotaka kugura Wasafi.

•Alisema kuwa hajalishwi na maneno ya uongo yanayoenezwa na wasanii ambao walitofautiana naye.

Diamond Platnumz na Harmonize
Diamond Platnumz na Harmonize
Image: INSTAGRAM//

Bosi wa WCB, Diamond Platnumz amefutilia mbali madai ya msanii wake wa zamani Harmonize kuwa alijaribu kuzuia nyota yake kung'aa.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Diamond alisema matamshi ambayo Harmonize alitoa mwaka jana baada ya kutua kutoka Marekani hayana ukweli wowote na yalikosa heshima.

Diamond alikana kuwahi kujaribu kumshusha Harmonize ama kumwagiza atoe kitita kikubwa cha pesa alipotaka kugura Wasafi.

"Hakuwa na heshima na maneno yake. Sikutaka kufuatilia sana. Kama aliongea hivo, mimi sikumkataza yeyote kuzungumza anachotaka. Naheshimu maneno yake, naheshimu kama kuna aliyeamini na ambaye hakuamini. Katika Wasafi, Hatuna mikataba ama mipango ya kumshusha tu," Diamond alisema.

Diamond aliweka wazi kuwa alipokuwa anaanzisha lebo ya Wasafi lengo lake lilikuwa kukuza wasanii wa Tanzania ila sio kumshusha yeyote.

Alisema kuwa hajalishwi na maneno ya uongo yanayoenezwa na wasanii ambao walitofautiana naye.

"Zamani ingetokea mtu aende kunizungumza vibaya nilikuwa naumia sana. Sasa hivi napuuza naona kama ni baraka. Sikutaka kufuatilia lakini mwisho wa siku kulizungumzwa. Watu walijua ukweli ni upi na uongo ni upi. Mimi kufikia hatua mpaka kutaka kumdhulumu mtu ama kumshusha, ni ya nini?. Hiyo ni kusema siamini katika mimi. Mimi naamini katika mimi. Siamini eti lazima nifanikiwe mpaka nimzidi mtu fulani," Diamond alisema.

Mbabe huyo wa muziki alimhimiza Harmonize na wasanii wengine wa kuacha kung'ang'ania ugomvi naye katika juhudi za kutafuta kiki.