Producer Master Jay asema Tz imeipiku Kenya kwenye burudani

Muhtasari

• Producer huyo alisema kwamba wasanii wa Tz wanajituma sana jambo ambalo limewafanya kuibuka kidedea.

• Alikiri kwamba kipindi cha nyuma kidogo, Kenya ilikuwa mbali sana ila mambo yamebadilika sasa.

Instagram, KWA HISANI
Instagram, KWA HISANI
Image: Master J

Producer mkali wa muziki kutoka Tanzania Joachim Marunda Kimaryo almaarufu Master Jay amesema kwamba Tanzania imeipiku pakubwa Kenya katika gemu la burudani.

Akizungumza katika mahojiano na wanahabari, Master alisema kwamba uchachari na kujituma kwa wasanii wa Bongo kumepelekea wao kuwa kifua mbele.

Alikiri kwamba kipindi cha nyuma, Kenya ilikuwa imeishinda Tz katika uzalishaji wa muziki ila kwa sasa mambo yamebadilika.

"...Acha nikuambie kitu na hata Kenya wenyewe wanajua. Kitambo sisi Tanzania tulikuwa tunatoa video kama za harusi, yaani Kenya ilikuwa mbali sana ila kwa sasa mambo yamebadilika sanaaa," Master Jay alisema.

Kulingana naye, Tanzania ipo mbele ya mataifa ya Uganda na Kenya katika upande wa muziki.

Aidha, alikiri kwamba kwa sasa wasanii wa Tanzania wanapigana kuhakikisha kwamba wanakubalika katika soko la ughaibuni jambo ambalo anaamini litatimia hivi karibuni.

Master Jay ambaye aliwahi kuwa msanii pia, alisema kwamba sasa ni nafasi ya chipukizi zaidi kutamba katika sekta hiyo na kuwa hatojihusisha kwenye masuala ya uimbaji kwa sasa.