"Silali kwa ajili yake!" Kipusa wa Mombasa aliyechorwa tattoo za Mbosso atua Tanzania kumsaka

Muhtasari

•Mariam amekiri kwamba tayari ametumia zaidi ya Ksh 40, 000 katika juhudi za kumtafuta msanii huyo.

•Mariam ametuma ombi kwa Mbosso apige hatua ya kumtafuta ili aweze kumkabidhi zawadi ambayo amemwandalia.

Image: HISANI

Mwanadada mmoja kutoka kaunti ya Mombasa amesafiri hadi nchini Tanzania akikusudia kukutana na 'crush' wake mwanamuziki Mbosso Khan.

Mariam ambaye amekuwa akifanya kazi Saudi Arabia tangu 2020 amekiri kwamba anampenda sana staa huyo wa Bongo na yupo hiari kufanya lolote kukutana naye kwa kuwa ana hamu kubwa ya kumuona.

"Namkubali sana Mbosso. Mimi ni kama shabiki wake. Yeye ndiye amenifanya nikatoka Uarabuni hadi Tanzania. Ugonjwa wangu ni kukutana na Mbosso. Nampenda sana sana!" Mariam alisema akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media.

Mwanadada huyo alitua Tanzania mnamo Machi 18 na amekuwa akitia bidii kubwa kukutana na Mbosso. Amekiri kwamba tayari ametumia zaidi ya Ksh 40, 000 katika juhudi za kumtafuta msanii huyo.

Amekiri kwamba alikuwa ameshindwa kuendelea na kazi yake nchini Saudi Arabia kwa sababu tu hajakutana na nyota huyo wa Bongo.

"Hata bosi wangu ananitafuta. Tuliagana nirudi Uarabuni kabla ya Ramadhan. Hata sijamjibu chochote kwa sababu nina umuhimu wa kumuona Mbosso ndio njiue kama nitarudi ama sitorudi. Kazi yenyeweilikuwa imenishinda," Alisema.

Mariam amefichua kwamba alianza kumfuatilia Mbosso miaka miwili iliyopita na tangu wakati huo upendo wake kwake umeendelea kukua.

Kutokana na mapenzi yake kwa Mbosso, Mariam amechora tattoo zake mbili kifuani na kwenye kiuno chake.

"Mbosso 4 life" Tattoo iliyo kifuani yasoma.

Kwenye kiuno chake Mariam amechorwa jina ya Albamu ya Mbosso, "Definition of Love"

Mariam ametuma ombi kwa Mbosso apige hatua ya kumtafuta ili aweze kumkabidhi zawadi ambayo amemwandalia.

"Nasumbuka sana Mbosso. Nina imani utaona mahojiano haya. Utie bidii uweze kunitafuta. Nina imani utapenda zawadi nilikuandalia. Nakupenda sana," Alisema.