Unachukua break ya miaka 10 tutakukumbuka vipi? Msanii Viviane amjia juu Sosuun

Muhtasari

• Mwanamuziki Vivianne ameonekana kukasirishwa na kitendo cha Sosuun kwenda kimya kwa muda mrefu.

• Ametaka wanawake wote kutokata tamaa baada ya changamoto katika maisha.

Instagram, KWA HISANI
Instagram, KWA HISANI
Image: Vivianne

Mwanamuziki Vivianne amemtupia cheche kali msanii mwenzake Sosuun kwa kile anachosema kwamba amezama kwa muda mrefu bila kutoa kibao licha ya kuwa na talanta ya kupigiwa mfano.

Kupitia ujumbe aliochapisha katika ukurasa wa Instagram, Vivianne alisema kwamba alimjua Sosuun enzile zile akiwa katika lebo ya Grandpa , ila inasikitisha kwamba staa huyo hasikiki tena.

"Nilimjua akiwa Grandpa, kwani mistari yake iliisha? Inasikitisha kwamba kipaji kama hiki kinaweza kupotea tu ghafla," Vivianne alisema.

Alisema kwamba Sosuun hakupaswa kuacha kuimba licha ya kujifungua mtoto, kwani hata yeye ni mzazi ila aliendelea kufukuzia ndoto na azma zake kimuziki na kimaisha.

Msanii huyo alisema itakuwa vigumu kwa mashabiki kumkumbuka Sosuun kwa sababu hakuacha kumbukumbu yoyote katika gemu la burudani.

Alimtaka msanii huyo kutumia talanta yake aliyopewa na Mungu na kukoma kuwa na visingizio vya mara kwa mara.

"...Mara ni bwana, mara ni watoto, mara wakwe zako. Unazama kwa miaka kumi, tutakukumbuka vipi jamani?" Vivianne aliandika.

Vivianne alisema kwamba wanawake wengi wanakata tamaa haraka sana baada ya kukumbana na changamoto za kimaisha.

Kama wosia wake kwa kina dada wote katika jamii, Vivianne aliwataka wanawake kujiepusha na 'ugonjwa' wa kukata tamaa maishani akitaja hali hiyo kuwa jambo lililopitwa na wakati.

Vivianne ni moja kati ya wasanii wa kike ambao wanajituma sana katika burudani la Kenya, huku akizidi kuwa kielelezo kw chipukizi wengi wanaolenga kujitosa katika muziki.