Khaligraph Jones atunga wimbo kumtaka rais Ruto kumlinda Raila dhidi ya matusi

Khaligraph Jones - Usiache Akemewe

Muhtasari

• Khaligraph alianza kwa kumpongeza Ruto na kumtambua kama mtu mcha Mungu.

• Alisema kuona Raila anakemewa mitandaoni kunampa msongo wa mawazo na kumtaka Ruto kuchukua hatua ya kumlinda dhidi ya kashfa hizo.

Msanii Khaligraph amemtaka Ruto kumlinda Raila kutoka kwa matusi
Msanii Khaligraph amemtaka Ruto kumlinda Raila kutoka kwa matusi
Image: Facebook, YouTube screengrab

Katika tukio lisilo la kawaida, msanii wa kutema mistari Khaligraph Jones ameachia wimbo kwa jina Usiache Akemewe.

Wimbo hu si wa kawaida kwa sababu msanii huyo ametumia weledi wake katika kuchana mishororo yenye vina vya tafsiri kutuma ujumbe kwa rais mteule William Ruto.

Khaligraph anaanza kwa kumpa pongezi za dhati rais Ruto na kisha kujikita katika maana halisi ya jina la ngoma yake ambapo anamuomba rais kumlinda aliyekuwa mshindani wake mzee Raila Odinga kutokana na kushambuliwa na watu.

Msanii huyo katika mistari yake anasikika akiimba kumtaka Ruto kumlinda Odinga kwa sababu yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kukomesha kauli na mashambulizi ya maneno yanayolenga kumdhalilisha Raila, haswa baada ya kushindwa urais kwa mara ya tano mfululizo.

“Kuna suala ambalo wewe pekee unaweza kulishughulikia, upatanisho; hiyo ndiyo tu tunayohitaji kuanza. Tulindie huyu mzee, usiache akemewe juu tunampenda vile tunakupenda, hatutaki kuona akikemewa na watu, wewe unajuwa ni nini amefanya, sisi tunajuwa ni nini amefanya,” Khaligraph Jones anaimba.

Jones anasema kwa sababu anajua Ruto ni Mkristo, anajua katika suala la upatanishi na kumlinda Odinga linawezekana.

Katika wimbo huo, anasema kwamba kila mtu anajua kile amabcho Odinga anapitia kwa sasa na kuona anasimangwa mitandaoni humpa msongo wa mawazo sana.

“Na wewe ni mtu wa Mungu kwa hivyo unajua jinsi ya kufanya vizuri zaidi. Juu saa hii wanatusi Raila na kuna uwongo usio na uhai, bwana hustler, ndio, mtu mwenye uadilifu huwaleta watu pamoja sababu chuki sasa hivi si kitu cha lazima. Ombi letu kama wananchi ni tuwekee Baba vizuri sababu najua unaelewa anachopitia huyo mzee” Jones alitema madini kwenye kipande hicho cha zaidi ya sekunde 127.

Jana pia msanii Justina Syokau aliachia kibao akimpongeza rais William Ruto huku akisema kwamba maombi ya Kenya yamejibiwa kwani uongozi wake ni Mungu amempa.