Amber Ray azungumzia picha yake akiwa kwa mganga na kuku wawili

Picha hiyo inamuonesha ameketi katika kilinge mikononi ana kuku wawili, mweusi na mweupe

Muhtasari

• “Niliiona kwenye mitandao ya kijamii na kila mtu mwingine, sikuwahi kujua kuwa picha kama hiyo ilikuwepo hapo awali" - Ray

Amber Ray azungumzia picha akiwa kwa mganga
Amber Ray azungumzia picha akiwa kwa mganga
Image: instagram

Kwa muda mrefu kumekuwa na picha yenye utata ya mwanamitindo Amber Ray akionekana ameketi kama vile kilingeni hivi kwa mganga akipigiwa ramli huku mikononi akiwa amewashika kuku wawili – mmoja mweupe na mwingine mweusi.

Katika kipindi chake cha As It Is kwenye YouTube yake, Amber Ray ameamua kulifungukia suala hili na kulainisha mambo, kutokana na maswali ya watu wengi ambao wengine wamekuwa wakilonga kwamba alienda kwa mganga kutafuta huduma kwa suluhu lake la kutodumu kwenye mahusiano.

Amber Ray aliamua kumwaga mtama kabisa kwa kusema kwamab picha hiyo kweli ni yeye wala hakuna uhariri umefanywa. Ila alisema kwamba mtu ambaye alimchukua kule kwa mganga ndiye yule yule aliyeichukua picha ile na kuanza kumtangazia kuwa alienda kwa mganga.

Amber ray akiwa kwa mganga
Amber ray akiwa kwa mganga

Picha hiyo mara ya kwanza ilisemekana kwamba Ray alienda kwa mganga ili kumtia ulozi mmoja wa wapenzi wake na yeye alifunguka kwamba huyo jamaa ndiye alimchukua kwa mganga.

“Niliiona kwenye mitandao ya kijamii na kila mtu mwingine, sikuwahi kujua kuwa picha kama hiyo ilikuwepo hapo awali. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, aliyenipiga ile picha nikiwa nimewashika kuku, yule yule niliyetuhumiwa nilienda kwa mganga kumroga, ndiye aliyenipeleka pale na kuipiga hiyo picha bila mimi kujua,” Amber Ray alisema.

Ray alisema kwamba hata yeye alishtuka kuiona picha hiyo kwenye mitandao na mpaka leo hii hajawahi kupata maelezo yeyote ni kwa nini jamaa huyo aliivujisha kwenye mitandao.

“Mimi nilihisi kwamba kuna kitu alikuwa anajaribu kunificha kwa sababu kila mara huwa tuko pamoja katika madhari mazuri lakini hunichukui picha, kwani mbona usubiri kunichukua picha katika mazingira kama yale,” Amber Ray alisikitika.