Kila mtu anataka kuwa kama mimi - Willy Paul

Pozee alisema kuwa wasanii wote sasa hivi wanamuiga si tu kimaisha bali pia kimuziki.

Muhtasari

• Kama sasa hivi wote wanangoja mimi nitoe kile kibao cha mwisho wa mwaka ndio wajue kama watatoa - Willy Paul.

Msanii Willy Paul na muonekano mpya mbele ya gari lake jipya aina ya Mercedes
Msanii Willy Paul na muonekano mpya mbele ya gari lake jipya aina ya Mercedes
Image: Instagram

Msanii wa kizazi kipya nchini Kenya Willy Paul amesema kuwa wasanii wenzake humu nchini wanamuiga katika kila kitu mpaka muda wa kutoa ngoma mpya bado wanafuata nyayo zake – asipotoa na wao hawatoi.

Kupitia instastory yake, Pozee aliwataka wasanii hao kukoma kumuiga katika kila kitu na kuenda mbele kuachia ngoma zao pasi na kungoja iwapo atatoa ndio wafuate nyayo.

Msanii huyo mwenye mikogo mithili ya tausi alisema kuwa wasanii wa humu nchini wanasubiria atoe kibao chake kikali kufunga mwaka ili na wao wato vyao.

“Kila mtu anataka kuwa kama mimi. Wote sasa wanaiga kile ambacho nakifanya. Kama sasa hivi wote wanangoja mimi nitoe kile kibao cha mwisho wa mwaka ndio wajue kama watatoa. Sawa, nyinyi toeni tu kwa sababu mimi nitatoa wakati najisikia,” Pozee alisema huku akijipiga kifua.

Msanii huyo ni hivi majuzi tu alijitunuku gari jipya aina ya Mercedes lenye rangi ya njano kwa kile alisema kwamba alihitaji kujipa zawadi kutokana na kutia bidi kimuziki mwaka huu akiachia vibao vyenye maudhui safi vilivyopata mapokezi mazuri na mashabiki wake ndani na nje ya nchi.

Pozee alidokeza kwamba zawadi hiyo ilikuwa ya kumpa moyo na kumhimiza kutobwaga manyanga hasa baada ya kile alikitaja kuwa madai ya uongo yaliyolimbikizwa dhidi yake na mwanablogu Diana Marua aliyesema kuwa msanii huyo alijaribu kumbaka – skendo ambayo nusra imtamatishie safari yake kimuziki.