Willy Paul apuuzilia mbali madai ya kutonunua gari la kifahari

Pozee aliwaonyesha watu magari yake yote ya kifahari anayomiliki

Muhtasari

• Willy Paul aliwaambia watu wajifunze kusherehekea mafanikio ya wengine na kuacha wivu.

Willy Paul

Staa wa muziki wa kizazi kipya Willy Paul amejibu madai ya baadhi ya wanamitandao kwamba alidanganya kuwa amenunua gari jipya.

Mjadala huu ulizuka baada ya Willy Paul kutangaza kununua gari la kifahari aina ya Mercedes Benz, la rangi ya manjano na wanamitandao kudai kuwa alipaka gari lake la kitambo rangi lionekane jipya.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Pozee alikana madai hayo huku akipakia video iliyoonyesha magari yake yote, kuanzia la kitambo, la sasa na matatu aliyonunua hivi majuzi.

"Walisema nilipaka gari langu la kitambo rangi ya manjano, hapana, magari yangu haya hapa yametulia. Maisha mazuri yasiyo na vikwazo maisha bila tata wowote," Pozee alijigamba.

Mwanamuziki huyo aliwashauri watu kuwatakia wengine mema na kutowaonea wivu wanapofanikiwa.

"Mjifunze kusherehekeana kwa sababu maisha ni mafupi na hayataki hasira, kwa hivyo mfurahie maisha ," Pozee alisema.

Alimshukuru Mungu kwa mafanikio yake mwaka huu na kwa kumjalia uwezo wa kujizawadi gari lingine.

"Mungu ametenda tena!!Asifiwe Mungu aliye juu. Asante Mungu kwa zawadi nyingine tena. Niliamua kujizawadi kwa kazi nzuri ambayo nimekuwa nikifanya na kwa kazi safi ambayo nimekuwa nikiwasilisha,nitaendelea vivyo hivyo," mwanamuziki huyo alisema.

Willy Paul aliwashukuru mashabiki wake kwa kumuunga mkono wakati wowote na ule wakati ambao watu walikuwa wanamkejeli.

"Na kwa mashabiki wangu ambao walinipa nafasi ya pili asanteni. Ni kwa sababu ya ukarimu wenu nimefika hapa," alisema.